Mkuu wa zamani wa usalama kuchaguliwa kiongozi Hong Kong
8 Mei 2022John Lee mwenye umri wa miaka 64, alikuwa mgombea pekee anayeungwa mkono na Beijing katika kinyang'anyiro cha kumrithi kiongozi anayeondoka Carrie Lam.
Kuchaguliwa kwake, kutamuweka afisa huyo wa usalama katika wadhifa wa juu kwenye kisiwa hicho kwa mara ya kwanza kufuatia miaka kadhaa ya mvutano wa kisiasa na vizuizi vya janga la ugonjwa wa UVIKO-19.
Soma pia:Hong Kong yapiga marufuku ndege kutoka nchi nane duniani
Kiongozi wa Hong huchaguliwa na kamati maalum ya uchaguzi, inayojumuisha watu 1,463 ambao ni takriban asilimia 0.02 ya idadi jumla ya wakaazi wa jiji hilo. Kamati hiyo, inayojumuisha wanasiasa wasomi na wafanyibiashara waliochaguliwa kutokana na utiifu wao kwa serikali mjini Beijing, watapiga kura leo Jumapili.
Lee anahitaji wingi mdogo tu wa kura, lakini bila ya kuwepo mpinzani, ushindi wake unaonekana kuwa dhahiri.
Kuliibuka maandamano makubwa ya kudai demokrasia mwaka 2019
Wachambuzi wanasema, kujitolea kwa John Lee kuzima maandamano ya kudai demokrasia kuliifanya China kumuamini, katika wakati ambapo wasomi wengi wa Hong Kongwalichukuliwa kuwa sio watiifu ama wasiokuwa na uwezo wa kutosha.
"John Lee anafahamika vizuri na serikali ya Beijing, kwa sababu alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na China bara," mbunge anayeiunga mkono China na mfanyibiashara maarufu Michael Tien ameliambia shirika la habari la AFP.
Lai Tung-kwok, waziri wa usalama wa Hong Kong kabla ya Lee kuchukua nafasi hiyo, ana mtazamo tofauti.
"Lee amefaulu mtihani," Lai ameiambia AFP. "Ikiwa anataka kitu kifanyike, anajitolea kadri awezavyo kukabiliana na vizuizi."
Lee anawakilisha mabadiliko katika uongozi wa kisiwa cha Hong Kong tangu mwaka 1997 kiliporudi kwa utawala wa China- viongozi wote wa zamani walikuwa wafanyibiashara ama watumishi wa umma.
Soma pia: Sheria ya usalama wa China kwa Hong Kong yazusha wasiwasi
Lee alihudumu katika idara ya polisi kwa miaka 35 kabla ya kuingia serikalini mnamo mwaka 2021, na kupandishwa cheo haraka katika kile vyombo vya habari kwenye kisiwa hicho vilivyokiita "lifti ya platinamu."
Chien-yu Shih, mtaalamu wa masuala ya usalama wa China katika taasisi ya ulinzi na usalama ya Taiwan, anasema Beijing ilianza kumtazama kwa jicho la karibu Lee baada ya maandamano makubwa ya kudai demokrasia ya mwaka 2019.
Maandamano hayo yalikuwa ni njia mojawapo ya waakazi wa Hong Kong kuonyesha hasira zao kwa kutokuwa na usemi kwa jinsi kisiwa hicho kinavyoendeshwa.
Maandamano yaliyoandaliwa na wanafunzi, waalimu, vyama vya wafanyikazi, madaktari na hata watumishi wa umma yalikuwa ni miongoni mwa maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa kisiwani humo kwa muda.
Hata hivyo, serikali ya China iliyaonyesha maandamano hayo kama yaliyochochewa na kuungwa mkono na mataifa ya kigeni, msimamo ulioungwa mkono na Lee.
"Beijing imekuwa ikitazama ni mwanasiasa yupo yuko tayari kusimama na China," Shih amesema, na kuongeza kuwa viongozi wa China bado hawana imani na watumishi wa umma kisiwani Hong Kong.