Mlinda lango Yann Sommer wa Uswisi astaafu soka la kimataifa
19 Agosti 2024Mlinda lango Yann Sommer wa Uswisi ametangaza kustaafu soka la kimataifa Jumatatu hii akiwa na umri wa miaka 35, na hivyo kuhitimisha maisha yake ya soka ya miaka 12 katika timu ya taifa.
Sommer ametandika daluga kwenye timu yake ya taifa baada ya kuichezea nchi yake michezo 94 tangu alipoanza kucheza mwaka 2012.
Sommer aliisaidia Uswisi kufika hatua ya robo-fainali katika michuano ya Yuropa mwezi uliopita na kupoteza kwa England waliomaliza katika nafasi ya pili kwa mikwaju ya penalti. Lakini pia aliwakilisha Uswisi kwenye hiyo ya Yuro mwaka 2016 na 2020, na vile vile Kombe la Dunia la 2018 na 2022.
Soma zaidi. Sommer aiacha Uswisi kwa ajili ya kuzaliwa kwa mtoto wake
Msimu uliopita Sommer alijiunga na Inter Milan ya Italia akitokea Bayern Munich ya Ujerumani.
"Baada ya kutafakari kwa kina, nimeamua kukatisha taaluma yangu kama golikipa wa timu ya taifa ya Uswisi," Sommer alichapisha kwenye Instagram.
"Pamoja na kuhitimishwa kwa duru nyingine kubwa ya fainali kwenye michuano ya Yuropa katika nchi jirani ya Ujerumani, ambapo hapo awali nilitumia miaka isiyosahaulika katika Bundesliga, wakati umefika wa kusema kwaheri."