Mmiliki wa vyombo va habari Hong Kong atiwa nguvuni
10 Agosti 2020Kulingana na msaidizi wake wa karibu Mark Simon aliyeandika kwenye ukurasa wa twitter, Lai alikamatwa mapema leo kwa madai ya kushirikiana na mataifa ya kigeni, na chini ya sheria hiyo mpya ya usalama hilo ni kosa. Simon ni afisa wa juu wa kampuni ya habari ya Lai ya Next Digital inayochapisha magazeti ya Apple Daily ambayo hukosoa vikali serikali ya Beijing na kuunga mkono demokrasia.
Gazeti la Apple Daily liliripoti kwamba Lai alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Ho Man Tin mapema leo. Gazeti hilo, limsema mtoto wake wa kiume Ian, pia alikamatwa akiwa nyumbani kwake.
Chanzo cha kipolisi ambacho kilizungumza lakini kwa sharti la kutotaja jina lake, kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba Lai alikamatwa kwa madai hayo ya kushirikiana na mataifa ya kigeni pamoja na udanganyifu. Hata hivyo, jeshi lenyewe halikuzungumzia mara moja taarifa hiyo.
Lai ni mtu wa kwanza mashuhuri kukamatwa hadi sasa chini ya sheria hiyo mpya ya usalama ya Hong Kong. Beijing ilianzisha sheria hiyo kuelekea Hong Kong mwishoni mwa mwezi Juni, kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya kuipinga serikali mwaka jana.
Sheria hiyo mpya inazuia kile ambacho Beijing inakichukulia kama kujitenga, shughuli za kigaidi ama kile inachokiona kama uingiliaji wa nje katika mambo ya ndani ya Hong Kong.
Polisi sasa wana mamlaka makubwa ya kufanya msako bila ya waranti ama kuagiza watoa huduma za intaneti pamoja na majukwaa ya intaneti kuondoa jumbe zinazoonekana kama zinakiuka sheria hiyo.
Lai aliwahi kusema anajua atalengwa na sheria hiyo.
Lai aliibuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa demokrasia mjini Hong Kong baada ya machafuko ya Juni 4, 1989 yaliyosababishwa na hatua kali dhidi ya waandamanaji waliokuwa wanaunga mkono demokrasia, katika bustani ya Tiananmen, mjini Beijing.
Vyombo vya habari vya serikali vinamtaja Lai kama kiongozi anayeshirikiana na mataifa ya nje kuivuruga China Bara. Lai kwa pamoja na wanaharakati 14 wanaounga mkono demokrasia, anakabiliwa na madai ya kuandaa na kushiriki kwenye baadhi ya maandamano makubwa ya kuipinga serikali mwaka uliopita ambayo yalichukuliwa kuwa yalikuwa kinyume cha sheria.
Soma zaidi: China yatishia kuilipizia kisasi Marekani kuiunga mkono Hong Kong
Takriban watu wengine 10 wanatarajiwa kukamatwa leo, hii ikiwa ni kulingana na gazeti la mjini humo la South China Post, ingawa halikutaja chanzo cha taarifa hiyo.
Lai aliwahi kukamatwa mwaka huu kwa madai ya kuandaa kusanyiko kinyume cha sheria, pamoja na washirika wenzake wanaounga mkono demokrasia, wakihusishwa na maandamano ya mwaka jana.
Kwenye mahojiano na shirika la habari la Reuters mwezi Mei, Lai aliahidi kubaki Hong Kong na kuendelea kupambania demokrasia, ingawa alisema anatarajia kuwa mmoja ya watakaolengwa haswa na sheria hiyo mpya.
Mashirika: DW/DPAE