Mnada wa matangazo ya TV ya Bundesliga waanza
8 Juni 2020Mnada kwa ajili ya haki za kutangaza kwa njia ya televisheni duru ya pili ya Bundesliga unaanza leo ambapo kitengo cha kinachoendesha ligi ya Ujerumani DFL kinatarajia kukusanya mabilioni ya dola kutoka kwa watakaotoa ahadi mchakato ambao utaendelea hadi Juni 17. Ligi hiyo inapata zaidi ya asilimia 80 ya mapato yake kuptia matangazo ya televisheni pamoja na huduma za matangazo ya mtandaoni, ambapo huduma hizo zimeingiza kiasi cha euro bilioni 4.64 katika mapato ya misimu minne iliyopita kwa jumla. Mchakato huo ni kwa ajili ya msimu wa mwaka 2021/22 hadi 2024/25.
Michuano ya kombe la Ujerumani linarejea tena uwanjani bila mashabiki ambapo michezo ya nusu fainali itapigwa kesho Jumanne na Jumatano. Bayer Leverkusen inasafiri kwenda kuwakabili Saarbruecken ya daraja la nne, wakati Jumatano itakuwa zamu ya Bayern Munich kuoneshana kazi na Eintracht Frankfurt katika marudio ya fainali ya mwaka 2018 ambapo Bayern ilikubali kipigo cha mabao 3-1.