1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco: Ndoa za utotoni bado tatizo

20 Mei 2015

Ndoa za utotoni bado ni tatizo miongoni mwa jamii za kiislamu. Morchidat kundi la viongozi wanawake wa dini ya Kiislamu nchini Morocco wanaongoza mapinduzi ya kijamii kugombania haki za wasichana kupitia filamu.

https://p.dw.com/p/1FTLf
Marokko-Berlin Mode Ledertaschen
Picha: Andrea Kolb

Kikundi kijulikanacho kwa jina la morchidat ni kizazi kipya cha viongozi wanawake wa dini ya Kiislamu, ambacho ni sehemu ya vuguvugu la mapinduzi ya kimya ya kijamii yanayopinga ndoa za utotoni nchini Morocco.

Kikundi hicho cha viongozi wanawake wa dini kilianzishwa mwaka 2006, ili kupambana na Uislamu wa siasa kali kufuatia mashambulizi ya kujitoa muhanga yaliutikisa mji mkuu wa Morocco wa Casablanca mwaka 2003.

Katika jitihada zake za kupinga ndoa za utotoni kundi hilo limeandaa filamu ya kiengereza inayoitwa „Casablanca Calling“, inayoangazia ndoa za utotoni na ambayo ilionyeshwa rasmi katika mkutano wa kimataifa juu ya ndoa za utotoni mjini Casablanca.

Matumaini ni kwamba viongozi hao wanawake wa kidini wataweza kuhamasisha Uisilamu wa msimamo wa wastani pamoja na kusogeza mbele nafasi ya wasichana na wanawake katika jamii ya Morocco.

Yanayoangaziwa katika filamu ya Casablanca Calling

Marokko Frauen in El Aaiun
Wasichana nchini MoroccoPicha: Ane Nordentoft/Transterra Media

"Viongozi kama wa kundi la morchidat ni jaribio la nadra katika jamii ya kiislamu," amesema Merieme Addou mtengezaji wa filamu hio akizubgumza na shirika la habari la Reuters. Anaendelea kwa kusema, ni kwa mara ya kwanza katika nchi ya kiislamu jukumu la kidini kupewa mwanamke.

Miongoni mwa jitihada za kundi hilo la morchidat ni kutoa ushauri kwa wanawake na vijana katika misikiti, shule, nyumba za kutunza yatima, hospitali, magereza na maeneo mbalimbali ya vijijini.

Kipande kimoja cha filamu hiyo katika duka la sonara kinaonesha miongoni mwa mitazamo ya kijamii ambayo kundi la marchadat inajaribu kuiangazia.

Kipande hicho cha filamu kinamuonesha sonara mmoja nchini Morocco akimwambia mteja wake ambae alikuwa akinangalia vidani dukani mwake “Wasichana ni kama bomu linalosubiri kulipuka na kuharibu sifa ya familia,“ anaendelea kwa kusema suluhisho ni kuepukana na bomu hilo, kwa kuwaozesha wasichana wa kike mapema iwezekanavyo.

Mteja wake Hannane anamjibu kwa ukakamavu kuwa dini ya Kiislamu haihimizi ndoa za utotoni, na wanawake wanatakiwa kujihusisha na shughuli nyengine muhimu nje ya kazi za nyumbani.

Hannane anaendelea kusema katika filamu hiyo kuwa watu wa Morocco na nchi nyengine za kiislamu kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi katika hali ya ujinga na vilio, anaendelea kusema watu wengi kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakipinga haki za msingi za dini ya kiislamu kwa mwanamke.

Hannane anaoneshwa katika filamu akiwa msikitini anazungumza na mwanamke aliyekuwa akihadisia namna gani mjukuu wake wa miaka 14 anahangaika kupata mume,

Ingawa sheria ya Morocco hairuhusu msichana kuolewa chini ya miaka 18, ndoa za utotoni bado zimebaki kuwa tatizo.

Addou mtengezaji wa filamu hiyo anasema, mtazamo wake wa dini ya kiislamu ni tofauti na mtazamo wa watu wa magharibi. Wengi wanadhania Uilslamu ni dini inayokandamiza wanawake na kuwanyima uhuru, lakini ni tatizo la tamaduni na wala sio kutokana na Uislamu.

Anaongeza kwa kusema wanawake na wanaume ni sawa mbele ya dini ya Kiislamu, hakuna tofauti baina yao.

Mwandishi:Yusra Buwayhid/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman