1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yachagua viongozi wapya

8 Septemba 2021

Raia wa Moroko wanapiga kura Jumatano kuchagua wabunge na viongozi wa serikali za mitaa. Suala kuu katika uchaguzi huo ni wasiwasi kuhusu athari za janga la Covid-19 ambalo limezuia kufanyika kwa kampeni kubwa.

https://p.dw.com/p/404tW
Wahlen in Marokko | 2016
Picha: Jalal Morchidi/AA/picture alliance

Uchaguzi huo wa Jumatano ((08.09.2021)) unafanyika chini ya sheria mpya, ambazo wachambuzi wanasema zitaifanya kazi ya chama cha haki na maendeleo, JDP  kusalia madarakani - kuwa ngumu zaidi. Kuna wagombea kutoka vyama 31 vya kisiasa na miungano ambayo inawania viti 395 katika bunge. Pia watawachagua wawakilishi 678 wa mabaraza ya miji.

Chama cha PJD ambacho kimekuwa uongozini tangu mwaka 2011, kinatafuta kubaki madarakani kwa kipindi cha tatu. Kikiongozwa na waziri mkuu Saad-Eddine El Othmani, chama hicho kimefanya kampeini ya kuimarisha uchumi wa taifa hilo la kifalme. Hata hivyo, mabadiliko ya hivi karibuni katika sheria ya uchaguzi yanatarajiwa kupunguza ushawishi wa chama hicho, wakati ambapo nguvu za wabunge zimewekewa mipaka na nguvu za mfalme Mohamed Vl anayefanya maamuzi yote ya kimkakati.

Matokeo ya uchaguzi wa leo ni vigumu kutabiri kwasababu ya utafiti na maoni ya wapiga kura umepigwa marufuku. Ushindani unatarajiwa kuwa mkali na hakuna chama chochote kitakachopata ushindi wa dhahiri kukiwezesha kuunda serikali bila kutafuta muungano na vyama vingine.

Saad-Eddine El Othmani Außenminister Marokko
Waziri mkuu wa Morocco - Saad-Eddine El OthmaniPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Uchaguzi huo utafuatiliwa na waangalizi 4600 wa nchi hiyo na wengine 100 zaidi kutoka nje. Wapiga kura wengi wanatarajia kuwa mchakato huo wa uchaguzi utatoa suluhisho kwa matatizo ya nchi hiyo kutoka masuala ya ajira hadi kwa vizuizi vya virusi vya corona. Wagombea wameahidi kubuni nafasi za ajira na kuimarisha uchumi wa taifa hilo, elimu na huduma za afya. Moroko imeathirika pakubwa na janga la virusi vya corona lakini ina idadi kubwa zaidi ya watu waliopata chanjo barani Afrika kufikia sasa.

Kutokana na masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona katika taifa hilo, shughuli za kampeini zilizuiliwa na hilo lilitatiza juhudi za wagombea kufikia raia milioni 18 wenye sifa za kupiga kura. Badala yake, hali hiyo ilisababisha wawaniaji hao kuimarisha juhudi zao kupitia mitandao ya kijamii.

Wagombea pia hawakuruhusiwa kusambaza vijikaratasi na ikawabidi kuthibiti mikusanyiko yao ya kampeini kufikia wingi wa watu 25. Kulingana na takwimu kutoka kwa wizara ya afya ya Morocco, taifa hilo limerekodi zaidi ya vifo elfu 13 tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona. Huku taifa hilo la Morocco likiwa na moja ya uchumi thabiti zaidi na eneo la biashara lililoimarika la Casablanca, umaskini na ukosefu wa ajira pia vimekithiri hasa katika maeneo ya mashambani.

Morocco imeshuhudia maelfu ya vijana waliopoteza matumaini, wakifanya ziara za mara kwa mara katika maboti madogo kuelekea katika visiwa vya Canary nchini Uhispania ama kufikia eneo bara la Uhispania kupitia rasi ya Gibraltar.