MORONI : Umoja wa Afrika waanza vikwazo dhidi ya Anjouan
5 Novemba 2007Umoja wa Afrika umeanza vikwazo vya majini dhidi ya kisiwa kilichoasi cha Anjouan kwa kutumia wanajeshi wa Comoro na Tanzania wakiwa na bunduki za rashasha na zana za kufyetulia maroketi.
Vikwazo hivyo vya Umoja wa Afrika vilivyotangazwa mwezi uliopita vinajumuisha marufuku ya safari kwa baadhi ya maafisa wa serikali ya Anjouan mojawapo ya visiwa vitatu vikuu vinavyounda Comoro kwa sababu ya uchaguzi uliobishiwa hapo mwezi wa Juni ambao umemuweka rais wa kisiwa hicho Mohamed Bakar madarakani.
Francesco Madeira mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika kwa Comoro ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters mwishoni mwa juma kwamba hakuna chochote ikiwemo mizigo itakayoweza kuondoka au kuingia Anjouan bila ya kukaguliwa na kikosi cha Uchaguzi na Usaidizi wa Usalama cha Umoja wa Afrika ambacho kinapiga doria kwenye bahari.