1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa msituni wateketeza kusini magharibi mwa Ulaya

17 Julai 2022

Wimbi la joto kali la msimu wa kiangazi ambalo limesababisha matukio makubwa ya moto kote kusini magharibi mwa Ulaya linaendelea kusambaa

https://p.dw.com/p/4EFIn
Spanien | Waldbrände nahe Alhaurin de la Torre
Picha: Gregorio Marrero/AP Photo/picture alliance

Wimbi la joto kali la msimu wa kiangazi ambalo limesababisha matukio makubwa ya moto kote kusini magharibi mwa Ulaya linaendelea kusambaa, huku maeneo kadhaa ya bara hilo yakijiandaa kwa viwango vya juu vya joto mapema wiki ijayo.

Soma zaidi: Maelfu wazikimbia nyumba zao kuepuka moto wa msituni Ugiriki

Zima moto nchini Ufaransa, Ureno, Uhispania na Ugiriki wanapambana na matukio ya moto ya msituni ambao unateketeza maelfu ya hekta ya ardhi na kuwauwa maafisa kadhaa tangu mwanzoni mwa wiki.

Frankreich | Waldbrand in Landiras
Maelfu ya watu kusini mwa Ufaransa wahamishwaPicha: SDIS 33/AP/picture alliance

Ni wimbi la pili la joto kuyakumba maeneo ya kusini magharibi mwa Ulaya katika wiki kadhaa huku wanasayansi wakilaumu mabadiliko ya tabia nchi na kutabiri matukio zaidi ya mara kwa mara na makali zaidi ya hali mbaya kabisa ya hewa.

Nini kinatokea Ufaransa?

Zima moto katika mji wa pwani wa Arcachon katika jimbo la kusini magharibi la Ufaransa la Gironde wanapambana kuyadhibiti matukio mawili ya moto ya msituni ambao umeteketeza hekta 10,000 tangu Jumanne. Luteni Kanali Olivier Chavatte kutoka idara ya moto na uokozi amesema ni kazi ngumu kweli. Wamepeleka zima moto 1,200 na ndege tano kuukabili moto huo.

Tangu Jumanne, Zaidi ya watu 14,00 – wakaazi na watalii kwa Pamoja – wamelazimika kuondoka huku vituo vya muda vikitengenezwa kuwapokea wanaohamishwa.

Soma pia: Moto wa msituni watishia miundombinu Ugiriki na Uturuki

Mamlaka ya hali ya hewa ya Ufaransa inatabiri viwango vya hadi nyuzijoto 41 za Celsius katika maeneo ya kusini mwa Ufaransa Jumapili Pamoja na hadi nyuzijoto 35 kaskazini magharibi, huku viwango vipya vya juu kabisa vya joto vikitarajiwa Jumatatu.

Griechenland Ein Löschhubschrauber stürzt bei einem Lauffeuer auf der Insel Samos ab
Helikopta ya zima moto ilianguka baharini UgirikiPicha: Sofianos Drapaniotis/REUTERS

Nchini Ureno, taasisi ya hali ya hewa inatabiri hadi viwango vya nyuzijoto 42 za Celsius bila kupungua kabla ya wiki ijayo. Mkuu wa jeshi la ulinzi wa raia Andre Frenandes ameonya kuwa kitisho cha moto huo bado kipo juu mno. Katika kipindi cha wiki moja, watu wawili wameuawa na wengine Zaidi ya 60 kujeruhiwa. Zaidi ya hekta 15,000 za msitu na vichaka zimeteketezwa.

Serikali ya Lisbon ilitarajiwa kuamua Jumapili kama itarefusha hali ya dharura iliyotangazwa nchini humo.

Nini kinatokea Uhispania?

Nchini Uhispania, shirika la kitaifa la hali ya hewa limedumisha viwango kadhaa vya tahadhari kote nchini humo, kwa kuonya kuhusu viwango kufikia hadi nyuzijoto 41 za Celsius katika baadhi ya maeneo.

Serikali ya kikanda inasema matukio kadhaa ya moto wa msituni yaliteketeza jana maeneo tofauti ya nchi hiyo kuanzia kusini hadi Galicia katika upande wa kaskazini magharibi ambapo hekta 3,500 za misitu ziliharibiwa.

Mapambano dhidi ya moto wa msituno yamesababisha vifo vya maafisa kadhaa, kutoka kwa rubani aliyekufa wakati ndege yake ilianguka kaskazini mwa Ureno hadi kwa wawili waliokufa Ugiriki wakati helikota yao ilianguka baharini.     

Portugal | Waldbrände
Zaidi ya zima moto 1,500 wanapambana UrenoPicha: Patricia de Melo Moreira/AFP/Getty Images

Nchini Ugiriki, jeshi la ulinzi wa raia lilipambana kuzima moto uliokuwa unateketeza kisiwa cha Crete cha bahari ya Mediterania, wakati Morocco ikipambana na moto wa msituni katika milima yake ya kaskazini ambao umemuua mtu moja na kulazimu kuhamishwa kwa familia 1,000.

Nchini Uingereza mawaziri wa serikali wanatarajiwa kufanya kikao cha dharura. Mamlaka ya hali ya hewa ya Uingereza imesema viwango vya joto kusini mwa nchi hiyo huenda vikapindukia nyuzijoto 40 Jumatatu au Jumanne kwa mara ya kwanza, na kusababisha baadhi ya shule kuendelea kufungwa kwa wiki ijayo.

Meya wa London Sadiq Khan amewashauri wakaazi kutumia usafiri wa umma kama tu ni muhimu kusafiri. Kampuni za huduma za treni zimewaonya pia abiria kutosafiri.

AFP