Moukoko aweka rekodi wakati Dortmund ikipigwa na Union
19 Desemba 2020Matumaini ya Borussia Dortmund ya kushinda taji la Ligi Kuu ya Kandanda Ujerumani - Bundesliga yamepata pigo jipya jana usiku wakati walipofungwa 2 - 1 na Union Berlin katika usiku ambao mshambuliaji wao Youssoufa Moukoko alikuwa mfungaji wa kwanza mwenye umri mdogo kabisa katika historia ya ligi hiyo.
Moukoko ambaye ni mzaliwa wa Cameroon na mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani alifunga bao akiwa na umri wa miaka 16 na siku 28, na kuivunja kabisa rekodi ya awali iliyowekwa na Florian Witz wa Bayer Leverkusen ya miaka 17 na siku 34.
Dortmund wako katika nafasi ya nne, pointi sita nyuma ya vinara Bayer Leverkusen ambao watawaalika leo mabingwa Bayern Munich. Union Berlin wako katika nafasi ya tano pointi moja nyuma ya Dortmund. RB Leipzig ambao wako katika nafasi ya tatu, watacheza leo dhidi ya FC Köln mechi ambayo tutakuletea moja kwa moja leo jioni katika matangazo ya redio.