Mpaka wa Tanzania na Msumbiji wafunguliwa baada ya miaka 4
20 Machi 2024Hii ni baada ya mipaka hiyo kufungwa kwa zaidi ya miaka 4 kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama na vurugu zilizokuwa zikisababishwa na vikundi mbalimbali vya ugaidi nchini Msumbiji, ambavyo vilikuwa vinatumia mwanya huo kuingia nchini Tanzania.
Katika mahojiano na DW, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Mtwara, Dismas Mosha amesema, wasingeweza kufanya lolote kutokana na hali ilivyokuwa awali kwa sababu usalama wa raia ni kipaumbele kwa Serikali.
Serikali inalenga kuufungua uchumi
Ameeleza kuwa malengo ya serikali ni kuufungua kiuchumi mkoa wa Mtwara na kusini kwa ujumla, hivyo imeona ni vyema ni watu wanaoishi katika mikoa hiyo waweze kutoka nje, kutafuta fursa za kibiashara na kimaendeleo, kwa kuwa kufunguliwa kwa mpaka katika vituo vya Mkunya, Kilambo na Mtambaswala, kumeongeza idadi ya watu ambapo wastani wa watu 300 hadi 400 wanaingia na kutoka kwa siku mkoani hapa kwa sasa.
"Na niseme tu hatukufunga kabisa mpaka, tulighairisha tu shughuli kwa sababu ya upande wa pili kulikuwa na vurugu, unapomuhudumia mtu kutoka nje ya nchi anatakiwa aende kule ahudumiwe na serikali iliyopo, hasa upande wa pili kulikuwa na machafuko.” alisema Mosha.
Hata hivyo inaelezwa kuwa, idara zinazohusika na masuala ya ulinzi na usalama zimejipanga vizuri kuhakikisha ukaguzi makini unafanywa ili kutoruhusu mianya ya uhalifu kufanyika nchini hapa.
Kadhia hiyo imewaathiri watu kutokana na kukosa fursa ya kuingiliana kibiashara, kijamii na kimaendeleo na hata ukosefu wa huduma za afya. Kama inavyoelezwa na Juma Napinda- mtendaji katika chemba ya wafanyabiashara nchini.
"Ilipekelea biashara nyingi kufungwa, watu wengi walihama Mtwara, lakini sasa hivi suala la kufungua mpaka wa Mozambique, ni lango kubwa la kiuchumi kwa mkoa wetu wa Mtwara,” alisema Napinda.
Vijana kutojiunga na makundi ya ugaidi
Kwa upande wao wafanyabiashara wana maoni gani kutokana na hatua hiyo?
"Mimi mwenyewe binafsi ni mfanyabiashara wa vifaa vya uvuvi, mwanzo tulikuwa tunauza kabla ya mipaka kufungwa, lakini baada ya kufungwa mipaka kila kitu kilikata,” alisema Farid Said.
"Sasa hivi tunafanya vizuri kwenye biashara kwa sababu mwingiliano umekuwa mkubwa, kuliko hali ilivyokuwa mwanzoni wateja walikuwa hawaji kutoka Msumbiji,” Christina Chonde.
Aidha kwa upande wake afisa miradi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Global Peace Foundation linalofanya uhamasishaji utunzaji na ujenzi wa amani Benson Daudi- anasema licha ya kumalizika kwa vurugu katika taifa hilo jirani amewataka vijana kutoshawishika na kujiunga kwenye vikundi vya kigaidi na uhalifu.
"Na jamii na familia kwa ujumla, ni kuhakikisha kwamba wanafuata ile misingi yote ambayo inatakiwa waifuate na kuepuka kutumia ile mianya ambayo ni haramu,” alisema Daudi.
Akinukuliwa, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara katika mikoa hii ya kusini mwishoni mwa mwaka jana, alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Msumbiji kimeshuka kutoka shilingi bilioni 53 hadi kufikia shilingi bilioni 26 katika kipindi cha mwaka huo na kuahidi kuongeza uwekezaji pamoja na kulifanyia kazi eneo hilo muhimu.