Mpambano wa sera na taswira
10 Septemba 2013Peer Steinbrück ni mtaalam wa masuala ya fedha na anaitambua vyema mizigo inayoikaba bajeti ya serikali kuu. Aliwahi kuwa waziri wa fedha katika serikali ya muungano wa vyama vikuu iliyokuwa ikiongozwa na Angela Merkel, lakini sasa anataka kumrithi mkuu wake wa zamani.
Anataka kuwa kansela. Lakini pambano hilo linaonyesha si sawa. Steinbrück anapambana na ukuta - hiyo ndio sura inayojitokeza.
Kwa mujibu wa wachunguzi wa maoni ya umma, Steinbrück hafui dafu mbele ya Kansela Merekel na hali hiyo imeanza tangu alipoteuliwa. Sababu za hali hiyo ziko nyingi tu: Merkel anang'ara kileleni mwa madaraka yake, anakidhibiti chama chake na katika suala la jinsi ya kusimamia mzozo wa Euro na madeni, sauti yake ina uzito mkubwa katika siasa za Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
"Wengi wa Wajerumani wanamheshimu na kummezea mate. SPD na Steinbrück hawawezi kushindana na hali hiyo. SPD wanazungumzia yale yote ambayo hayendi vizuri," anahoji mtaalam wa masuala ya mawasiliano Christoph Moss.
Kwa wapigakura wa SPD, hayo hayatoshi, anahisi. Na hayaambatani na hali ya mambo hasa kwa sababu "Wajerumani wanaonesha wameridhika sana hivi sasa." Wapigakura wanataka kujua mengi zaidi, kipi Steinbrück na chama chake watakifanya bora zaidi pindi wakishinda uchaguzi.
Sera za mageuzi za Schröder zinamsaidia Merkel na sio Steinbrück
Steinbrück na chama chake cha SPD wangekuwa na ya kutosha kuwatanabahisha wapiga kura .Lakini ni mada ambazo hazipendwi. Ajenda ya mageuzi ya Gerhard Schröder, aliyekuwa kansela kabla ya Angela Merkel, mashuhuri kwa jina la Ajenda 2010, inaangaliwa na wataalamu kuwa ndio msingi wa nguvu ilizonazo Ujerumani katika wakati huu wa migogoro ya madeni ulimwenguni.
Walikuwa SPD walioanzisha ajenda hiyo inayopunguza gharama za huduma za jamii, licha ya upinzani chamani. Mfumo wa bima ya jamii ukawa ghali, malipo ya wasiokuwa na kazi yakapunguzwa, umri wa kustaafu ukarefushwa - kwa ufupi serikali ikapunguziwa gharama.
Makali hayo yamewaathiri zaidi wafuasi wa chama cha SPD. Wengi wakakipa kisogo chama hicho. Uchaguzi unapoitishwa wapiga kura wa SPD huona bora wasalie majumbani mwao.
Hivi sasa SPD wanajuta, anahisi Edgar Wolfrum, mtaalam huyo wa fani ya historia katika chuo kikuu cha Heidelberg. "Tatizo ni kwamba ,SPD wanajitenganisha wenyewe na matokeo ya ufanisi wa serikali yao."
Mtaalamu huyo wa historia anaitaja hali hiyo kuwa ni sawa na "kutohalalisha siasa waliyoifuata kati ya mwaka 1998 na 2005."
Peer Steinbrück alikuwa na anaendelea bado kupigania sera za mageuzi katika huduma za jamii, sera ambazo hivi sasa takriban kila chama kinakiri hazina mbadala.
Kiroja lakini ni kwamba sera hizo zinaungwa mkono zaidi na vyama vyengine vinavyotambulika kuliko na chama cha SPD. Merkel anafaidika na ile hali kwamba SPD imeifanya serikali iwe na nguvu kuweza kukabiliana na migogoro ya fedha.
Msimamo wa wastani wawaniwa
Tofauti zipo na zinakutikana katika muongozo wa uchaguzi. SPD wanataka pawepo kiwango cha chini cha mishahara - yaani Euro nane na senti 50 kwa saa moja, lakini ndugu vya CDU/CSU lakini vinapinga.
Vyama vinavyopigania masilahi ya wafanyakazi vinatakiwa vibuni kiwango cha chini cha mshahara bila ya akuwepo muongozo wa kisheria. Katika asuala la kodi za mapato, SPD wanataka matajiri wawajibike. CDU/CSU wanataka madeni ya serikali yapunguzwe - wanataka pia kukwepa kupandisha kodi za mapato, ingawa wanataka gharama ziongezwe.
Takriban vyama vyote vya kisiasa vinapigania wapiga kura wa wastani.
Hofu kubwa lakini walizo nazo wanaasiasa wa vyama vyote zinahusu idadi ya wale wanaokwepa kupiga kura. Idadi yao imeongezeka mara tatu tangu miaka ya 70.
Takriban asilimia 30 ya watu wenye haki ya kupiga kura wamekwepa kuitumia haki yao hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009. Na katika chaguzi za majaimbo idadi ya wanaoona bora waasiteremke vituoni kupiga kura hufikia asili mia 40. Kama zamani vijana ndio waliokuwa wakilaumiwa kuwa wavivu wakupiga kura,hivi sasa hirimu zote zinahusika.
Mwandishi: Wagener Volker/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo