1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa EU wa kufufua uchumi unaelekea kufikiwa

Admin.WagnerD20 Julai 2020

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wameelezea matumaini yenye shaka shaka ya kufikiwa makubaliano ya mpango wa uokozi wa uchumi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/3fbqO
EU-Gipfel Coronavirus | Angela Merkel, Emmanuel Macron und Charles Michel
Picha: picture-alliance/abaca/Monasse T/ANDBZ

Mazungumzo magumu yanaendelea mjini Brussels huku rais Macron akisema kuna matumaini ya viongozi vigogo kulegeza kamba ili kufikia makubaliano lakini ameonya kwamba hakuna uamuzi wowote uliofikiwa hadi sasa na yungali anajizuia kutoa matamshi ya kutia moyo.

Macron ameeleza hayo wakati viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya walipoanza kukusanyika kwa awamu nyingine ya mazungumzo baada ya siku tatu za mwanzo za mkutano kukamilika bila ya kuwepo mwafaka kuhusu mpango wa ufufuaji uchumi wa Euro bilioni 750.

Rais Macron na Kansela Merkel, viongozi wawili wenye nguvu ndani ya kanda ya Umoja wa ulaya wanaunga mkono mpango huo lakini wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka Uholanzi na nchi nyingine tajiri za kaskazini ya Ulaya zilizopachikwa jina la "Mataifa Bahili"

Akielezea matumaini yake ya kufikiwa makubaliano kansela Merkel amesema "Jana usiku, baada ya majadiliano marefu tumepata njia ya kufikia makubaliano. Hiyo ni hatua nzuri na tuna imani kwamba tunaweza kufikia makubaliano leo au hata kuona kuwa makubaliano yanawezekana."

Von der Leyen aelezea matarajio yake 

EU-Ratspräsidentschaft Deutschland | PK Ursula von der Leyen & Angela Merkel
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen Picha: Reuters/J. Thys

Matumaini kama hayo yameelezwa pia na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ambaye amesema anatarajia maafikiano na kwamba majadiliano yanaelekea upande unaotia moyo.

Von der Leyen amewatolea wito viongozi wa Umoja wa Ulaya kumaliza tofauti zao na kuwezesha kupatikana makubaliano akisisitiza kuwa raia wa kanda ya Ulaya wanataka majibu ya mzozo unaowakabili na jinsi ya kujitayarisha kwa siku zijazo.

Kwa lengo la kuishawishi Uholanzi kuunga mkono mpango huo, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel alitarajiwa kupendekeza kupunguza kiwango cha misaada ambacho kingetolewa kupitia mpango wa uokozi kutoka Euro bilioni 500 hadi Euro Bilioni 390.

Matumaini yametolewa pia na upande wa upinzani 

Präsidentenpalast in Bogor  West Java  Indonesia
Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte Picha: Kris

Uholanzi na mataifa mengine pinzani yanataka sehemu kubwa ya fedha za mfuko wa uokozi zisitolewe  kama misaada na badala yake iwe mikopo ambayo nchi wanachama zitakazonufaika zitalazimika kuzilipa miaka michache ijayo. 

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amenukuliwa akisema inawezekana kupata maelewano ya jinsi ya kuutanzua mvutano uliopo na kuongeza kwamba hatua muhimu imepigwa katika mazungumzo ya siku tatu zilizopita.

Hayo yakijiri Bunge la Ulaya limeonya kuwa halitouunga mkono mkataba wowote  utakaofikiwa na viongozi wakuu wa kanda hiyo iwapo utashindwa kutimiza masharti kadhaa.

Wabunge wa Umoja wa Ulaya wanataka mpango utakaopitishwa ujumuishe masharti ya kulinda utawala wa sheria na uwezekano wa kuzuia msaada wa kifedha kwa mataifa wanachama yanayokiuka misingi ya kidemokrasia.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Josephat Charo