1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kudhibiti uhamiaji wa watu kuelekea Ulaya

29 Agosti 2017

Wakuu wa Umoja wa Ulaya na nchi 3 za Afrika wakubaliana kuhusu mpango wa kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoelekea Ulaya, na pia kukabiliana na uhamiaji haramu

https://p.dw.com/p/2j0o1
Frankreich PK Migrationsgipfel in Paris
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Mataifa manne ya Ulaya yenye ushawishi mkubwa katika bara hilo pamoja na nchi tatu za Afrika zimekubaliana kwenye mpango wa kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu na pia kuunga mkono mataifa yanayolemewa na uhamiaji wa watu kupitia jangwa la Afrika na pia kupitia bahari ya Mediterania.

Kwa muda mrefu, Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 umekuwa ukijizatiti kupata suluhisho muafaka kuhusu mzozo wa ongezeko la wahamiaji wanaokimbia vita, umaskini na misukosuko ya kisiasa katika Mashariki ya Kati na bara la Afrika, mzozo ambao sasa unatishia ushirikiano kati ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Akiwa mwenyeji wa mkutano ambao umewaleta pamoja  wakuu wa nchi za Ujerumani, Italia, Uhispania, Chad, Niger na Libya kujadili suala hilo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa wakati umewadia wa kuwa na mpangilio imara.

Gharama ya wahamiaji yazua mgongano

Wahamiaji waliojazana kwenye boti ya raba/mpira waonekana baharini karibu na ufuo wa Libya
Wahamiaji waliojazana kwenye boti ya raba/mpira waonekana baharini karibu na ufuo wa LibyaPicha: picture alliance/dpa/NurPhoto/C. Marquardt

"Ninataka kusema kuwa mpango huu wa muda mfupi ambao tumeweka, ninafikiria ndio wa dharura lakini suluhisho madhubuti kwa yale ambayo tumekuwa tukishuhudia katika miezi michache iliyopita na ambayo hayakubaliki. Ukweli ni kuwa wasafirishaji haramu ambao ni walanguzi wa silaha na ambao wamegeuza jangwa la Afrika kuwa makaburi na kugeuza Mediterania kuwa makaburi ndio wale wanaohusishwa na ugaidi."

Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania zimekubaliana  kuzisaidia Chad na Niger kuimarisha udhibiti katika mipaka yao ili kuzuia idadi ya watu wanaofanya safari ya hatari kupitia bahari ya Mediterania. 

Suala la wahamiaji limeziweka Ufaransa na Italia katika mgongano, huku Italia ikiilaumu Ufaransa na nchi wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya kwa kutosaidia katika kubeba mizigo ya wahamiaji, na imeiomba tume ya Umoja wa Ulaya kuongeza bajeti ili kusaidia kushughulikia mzozo huo.

Utambulisho wa wahamiaji halali na haramu

Viongozi hao wamekubaliana kwa mpango wa kuanza kuwatambua wahamiaji halali wanaokimbia vita au waliopo katika kitisho cha kuuawa na kutumia Umoja wa Mataifa kuwasajili nchini Niger na Chad kama hatua ya kuwazuia dhidi ya unyanyasaji kutoka kwa wasafirishaji haramu wa binadamu. Mapendekezo yanaweza kushuhudia utekelezaji bora wa sheria dhidi ya wasafirishaji haramu wa watu.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakiwa Paris
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakiwa ParisPicha: Reuters/C. Platiau

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel anasisitiza kuwa dhamira kuu ni kukabiliana na uhamiaji haramu."Ufaransa imewasilisha baadhi ya mapendekezo, Shirikaka la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR  litashiriki, bila shaka tutawapa mustakabali hawa wakimbizi, lakini hilo litawezekana tu ikiwa tutaweza kutofautisha kati ya wakimbizi halali na wale wa kiuchumi wanaotaka kuingia Ulaya kupitia fukwe za Ulaya kutoka Libya."

Mwaka huu pekee, takriban wahamiaji 120, 000 wameingia Ulaya miongoni mwao wakimbizi kupitia njia ya bahari. Kulingana na shirika la Kimataifa kuhusu wahamiaji, zaidi ya watu 2, 400 wamekufa maji wakiwa katika safari hiyo hatari ya kuhama, ambayo aghalabu hufanywa na wasafirishaji haramu wa binadamu.

Rais wa Chad Idriss Deby amesema kuwa wanafanya kila waliwezalo kupunguza hasara na vifo vya Waafrika katika jangwa au baharini wanapojaribu kuvuka bahari. Mkuu wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa pia alikuwapo katika mazungumzo hayo mjini Paris.

Kikao hicho ambacho si rasmi hakikuelezea kinaganaga mikakati mipya ya ufadhili wa mpango waliotilia saini. Huku maelfu ya wakimbizi wakifika Libya kabla ya kuanza safari yao kuelekea Ulaya, viongozi hao walisisitiza kuwa kuifanya Libya kuwa thabiti ndiyo itakuwa jambo la msingi katika kutafuta suluhisho la kudumu.

Mwandishi: John Juma/RTRE/DPAE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo