Mpango wa kupambana na Ebola wazinduliwa
1 Agosti 2014Hayo yanajiri wakati kukiandaliwa mkutano wa kilele unaozijumuisha nchi za eneo hilo ili kuzindua mpango mahsusi na wa dharura ili kukabiliana na hali hiyo. Viongozi wa nchi nne za Afrika Magharibi -- Guinea, Sierra Leone, Libera na Cote d'Ivoire – wanakutana leo katika mji mkuu wa Guinea, Conakry, pamoja na kiongozi wa Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, Margaret Chan, ili kuzindua mpango wa pamoja wa kiasi cha dola milioni 100 zilizotengwa maalumu kupambana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa hatari wa Ebola.Msemaji wa Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO, Paul Garwood anafafanua kuhusu mpango huo.
"Mpango huo unawajumuisha maafisa wa matibabu watakaosaidia kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo. Wao ni pamoja na madkatari, wauguzi, mabingwa wa milipuko ya magonjwa, wataalamu wa mawasiliano na wahamasishaji watakaozungumza na watu katika jamii ili kuwapa ujumbe wa hatua za kuchukua, kutembelea vituo vya afya na kuhakikisha kuwa wanapata matibabu ya mapema".
Mkutano huo wa kilele unaandaliwa wakati maafisa wa afya wa Marekani, Ujerumani na Ufaransa wakitoa tahadhari kwa raia wake kutosafiri katika nchi zilizoathirika – Guinea, Liberia na Sierra Leone – ili kuuzuia ugonjwa huo kusambazwa katika nchi zao.
Hospitali moja kusini mwa Marekani imesema inajiandaa kumpokea mgonjwa mmoja aliye na virusi vya Ebola, katika siku chache zijazo, ili apokee matibabu katika mojawapo ya vyumba maalum.
Wakati huo huo, Nigeria imewaweka watu wawili katika eneo maalum ambao miili yao iligusana na wa mwanamme mmoja aliyefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola mjini Lagos wiki iliyopita, wakati Afrika Magharibi ikikabiliana na hali hiyo ambayo ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa. Guinea, Liberia na Sierra Leone zinajitahidi kuuangamiza ugonjwa huo ambao umewaambukiza zaidi ya watu 1,300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na kutishia kusambaa katika nchi nyingine.
Shirika la Afya Ulimwenungi – WHO limesema idadi ya vifo kutokana na Ebola imepanda hadi 729 baada ya watu wengine 57 kufariki. WHO imetangaza kuwa visa vingine vya maambukizi vipatavyo 122 vimegundulika kati ya Alhamisi na Jumapili wiki iliyopita. Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma alitangaza hali ya hatari na akafuta ziara yake ya Washington wiki ijayo ambapo viongozi 50 wa Bara Afrika watakutana na Rais Barack Obama.
Sierra Leone, ambayo imewapoteza raia wake 233, imemzika jana daktari wake Umar Khan, aliyetajwa kuwa “shujaa wa kitaifa” ambaye aliyaokoa maisha ya zaidi ya wagonjwa 100 wa Ebola kabla ya kufariki kutokana na ugonjwa huo. Tangazo limekuja siku moja baada ya Liberia, ambayo imewapoteza watu 156, kufunga shule zote.
Hofu kuwa ugonjwa huo unaweza kusambaa katika mabara mengine kupitia safari za ndege imekuwa ikiongezeka, huku nchi za Ulaya na Asia zikiwa katika hali ya tahadhari pamoja na nchi za Afrika zilizo nje ya eneo lenye mgogoro huo wa Ebola. Nchini Uingereza, mwendesha baiskeli wa Sierra Leone Moses Sesay alipimwa virusi vya Ebola katika michezo inayoendelea ya Jumuiya ya Madola mjini Glasgow, kabla ya kuruhisiwa kushiriki.
Shirika la hisani la Madaktari wasio na Mipaka limeonya kuwa mgogoro huo unaendelea kuwa mbaya zaidi likisema kuwa hakuna mkakati madhubuti uliowekwa katika kuukabili mlipuko wa ugonjwa huo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel