1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mpango wa Sunak wakuwapeleka wahamiaji Rwanda wafanikiwa

Saleh Mwanamilongo
18 Januari 2024

Bunge la Uingereza limepitisha muswada tata wa Rishi Sunak wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda, zoezi ambalo hata hivyo limezua mpasuko katika chama chake.

https://p.dw.com/p/4bPEm
Muswada wa Sunak wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda wapita Bungeni
Muswada wa Sunak wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda wapita BungeniPicha: UK Parliament/Roger Harris/REUTERS

Wabunge 320 walipiga kura ya ndio huku 276 wakipiga kura ya hapana kupinga mswada huo wa sheria ya waomba hifadhi. Kura hiyo ilikuja siku moja baada ya wabunge 60 wa chama tawala cha Wahafidhina cha Waziri Mkuu Sunak kutangaza kuwa watapiga kura ya kupinga mswada huo wa sheria.

Mzozo huo ulisababisha pia manaibu wawili wa chama chake cha kihafidhina kujiuzulu na kutangaza kupinga mpango huo. Lakini wakati wa upigaji kura bungeni, ni wabunge 11 pekee wa chama cha Kihafidhina waliopinga mswada huo wa sheria.

''Kuingia Uingereza kinyume cha sheria huwezi kukaa''

Wachambuzi wamesema endapo uasi huo ungendelea hapo jana Jumatano basi ungehatarisha mpango wa Waziri Mkuu wa kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi nchini Uingereza na pia kuyumbisha serikali ya Sunak ambayo ina miezi 15 pekee madarakani.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly amesema msuada huo wa sheria unalenga kuhakikisha usalama wa raia wa Uingereza.

"Muswada huu unatoa ujumbe wa wazi usio na utata kwamba ukiingia Uingereza kinyume cha sheria, huwezi kukaa. Mswada huu umeandaliwa kwa uangalifu mkubwa ili kusuluhisha na kufikisha mwisho changamoto za kisheria.", alisema Cleverly.

Sera yenye utata

Zaidi ya watu 30,000 waliingia Uingereza kinyume cha sheria 2023, kutoka 46,000 mwaka wote wa 2022
Zaidi ya watu 30,000 waliingia Uingereza kinyume cha sheria 2023, kutoka 46,000 mwaka wote wa 2022Picha: Jordan Pettitt/PA Wire/empics/picture alliance

Hivi sasa mswada huo wa sheria utawasilishwa kwenye baraza la seneti, ambapo unakabiliwa na upinzani zaidi. Chama tawala hakina uwingi kwenye baraza hilo la Seneti. Maseneta wanaweza kuchelewesha na kurekebisha sheria lakini hawawezi kubatilisha uamuzi uliofanyika na baraza la wawakilishi.

Mswada huo unalenga kushinda uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uingereza kwamba mpango wa kuwatuma wahamiaji wanaofika Uingereza kupitia mlango wa bahari Uingereza kwa boti hadi Rwanda, ambako wangekaa kwa kudumu, ni kinyume cha sheria.

Iwapo itaidhinishwa na Bunge, sheria itairuhusu serikali kufanya kuondoa sehemu za sheria za haki za binadamu za Uingereza ili kuruhusu waomba hifadhi kupelekwa Rwanda. Baadhi ya vipengee vya sheria hiyo vinazuia kupinga mahakamani kuhamishwa kwa wahamiaji.

Je, Rwanda yakerwa na siasa za Uingereza ?

Maafisa wa Rwanda wamekuwa wakionesha kuchoshwa na kile walichoelezea kuwa ni mchezo wa kuigiza wa Waingereza kuhusu mpango wa kuhamishwa waomba hifadhi. Rais Paul Kagame alisema ni tatizo la Uingereza na si tatizo la Rwanda ikiwa waomba hifadhi hawatopelekwa Rwanda. Kagame aliliambia shirika la habari la BBC kwamba kama waomba hifadhi hawatapelekwa Rwanda, basi nchi yake iko tayari kurudisha pesa za Uingereza. Uingereza na Rwanda zilitia saini mkataba wa kuahidi kuimarisha ulinzi kwa wahamiaji.