Mpasuko mkubwa waitikisa serikali Ujerumani
14 Juni 2018Mgogoro kuhusu sera ya uhamiaji nchini Ujerumani unazidi kuleta taharuki kati ya Kansela Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya ndani Hörst Seehofer. Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yameshindwa kupata mwafaka. Seehofer anasisitiza juu ya ulazima wa kuwa na ukaguzi mkali mipakani wakati Kansela Merkel anatilia mkazo wa kutafutwa mkakati utakaomulika kanda nzima ya Umoja wa Ulaya.
Serikali mpya ya muungano nchini Ujerumani haijatimiza hata siku 100 lakini mapambano yameshaanza kuitikisa,na sababu kubwa ni sera ya uhamiaji. Mapambano hayo yanatishia kuuongeza mgawanyiko ndani ya kundi la vyama vya kihafidhina yaani chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic na chama ndugu cha CSU,Christian social Union. Chama cha CSU kinatia msukumo wa kuzingatiwa msimamo mkali zaidi kuhusu suala la wahamiaji mwelekeo ambao unashikiwa bango na kiongozi wake Hörst Seehofer ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani.
Pendekezo la chama hicho ni kwamba polisi wanaosimamia mipaka ya Ujerumani wapewe mamlaka ya kuwarudisha walikotoka wakimbizi wanaokuja kutafuta kuomba hifadhi Ujerumani licha ya kwamba wameshajisajili katika nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya au wakimbizi wasiokuwa na vitambulisho.Kundi la Kansela Merkel kwa upande wake halikubaliani na sera hiyo badala yake linataka Ujerumani isichukue uamuzi wa peke yake wa kuwatimua watu mpakani kwasababu kwa mtazamo wao hatua hiyo itahujumu mshikamano wa Umoja wa Ulaya na kuleta matatizo na Austria ambayo itahitajika kubeba mzigo wa kuwapokea wakimbizi waliokataliwa. Merkel na kundi lake wanataka mpango wa pamoja wa Umoja wa Ulaya kuhusu sera ya uhamiaji ambayo itaridhiwa nchi zote za jumuiya hiyo katika mkutano wa kilele baadae mwezi huu.
"Kwangu mimi suali kuhusu tutakavyolitatua tatizo la wahamiaji ni jambo ambalo ni mtihani kwa hatima na mshikamano wa Ulaya. Na maslahi ya kila nchi lazima yazingatiwe.
Duru zinasema Seehorfer huenda akamkiuka Merkel na kushinikiza kivyake juu ya mageuzi ya sera ya uhamiaji katika Umoja wa Ulaya. Leo unafanyika mkutano mwingine kati ya Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo na suala hilo la sera ya uhamiaji ndio agenda kuu. Inaarifiwa kwamba sasa Kansela Merkel anaonekana kulegeza msimamo akisema kwamba huenda polisi inaweza kupewa mamlaka mapya kuwafukuza watu mpakani ambao waliwahi kunyimwa hifadhi. Chama cha CSU kimesema kiko tayari kumuunga mkono Merkel katika juhudi zake za kushinikiza mageuzi hayo katika ngazi ya Umoja wa Ulaya ikiwa ataridhia ombi lao hilo la kuwatimua wakimbizi mpakani kurudi kwenye nchi walikojiandikisha mwanzo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman