1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mpinzani mkubwa wa China kuwania urais Taiwan

12 Aprili 2023

Chama tawala cha Taiwan kimemteua Makamu wa Rais William Lai kuwania urais mwakani, akiwa mwanasiasa mwenye msimamo mkali zaidi dhidi ya China kuliko rais wa sasa, Tsai Ing-wen, hatua inayotishia kuzidisha uhasama.

https://p.dw.com/p/4PwWc
Taiwan | Lai Ching-te
Picha: Ceng Shou Yi/NurPhoto/picture alliance

Tangazo hilo la leo (Aprili 12) la chama cha Democratic Progressive, DPP, limetolewa siku mbili tu baada ya China kusema imekamilisha rasmi mazoezi yake ya kivita dhidi ya kisiwa cha Taiwan, mazoezi ambayo yaliashiria uwezo wake wa kukivamia na kukizingira kisiwa hicho.  

Lai anafahamika kwa misimamo yake mikali na ya wazi juu ya uhuru kamili wa Taiwan na kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kunaweza kuchukuliwa kama tangazo la kuongeza uhasama dhidi ya China.

Soma zaidi: Rais wa Taiwan akosoa mazoezi ya kijeshi ya China

"Nimeupokea kwa heshima kubwa uteuzi wa DPP kushiriki kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2024 na kubeba jukumu la kuilinda Taiwan." Alisema Lai wakati akizungumza mbele ya vyombo vya habari hivi leo.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63 amekuwa akitazamiwa kuwa mrithi wa Tsai, ambaye anamaliza muhula wake wa vipindi viwili vya miaka minne minne ifikapo Mei mwakani.

Msimamo mkali wa Lai

Msimamo wa Lai ni kwamba Taiwan haiwezi kamwe kuwa na amani ya kudumu kwa kuendelea kuiridhisha China na amekuwa akiwatolea wito raia wa kisiwa hicho kuungana dhidi ya kile anachokiita utawala wa kikatili wa China.

Taiwan Neujahr 2022 Tsai Ing-wen
Rais wa sasa wa Taiwan, Tsai Ing-wen (kulia), akiwa na makamu wake, William Lai, mwaka 2022.Picha: Taiwan Presidential Office/REUTERS

Soma zaidi: Tsai:Mazoezi ya kijeshi ya China yameondoa utulivu wa kikanda

"Sasa, kundi la mataifa ya kidemokrasia duniani limekitambua kitisho cha China kwa jamii ya kimataifa na linaguswa na umuhimu wa amani ya Mlango Bahari wa Taiwan. Lazima mujitayarishe na vita ili kuepuka vita, ili kuzuwia vita lazima muwe na uwezo wa kupigana vita." Aliwaambia waandishi wa habari nje ya makao makuu ya chama cha DPP mjini Taipei.

China kutangaza eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka

Uteuzi wa Lai unakuja siku ambayo wizara ya ulinzi ya Taiwan imetangaza kuwa China ilikuwa inapanga kutangaza eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka lenye ukubwa wa maili 85 kwenye bahari ya kaskazini mwa kisiwa hicho, ikithibitisha ripoti iliyowahi kuandikwa awali na shirika la habari la Reuters juu ya uwezekano wa China kulifunga anga la Taiwan.

Taiwan | Lai Ching-te
Makamu wa Rais wa Taiwan, William Lai, aliyeteuliwa kuwania urais kwenye uchaguzi wa Mei 2024.Picha: Ceng Shou Yi/NurPhoto/picture alliance

Soma zaidi: China yahitimisha luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan

Taiwan inasema hatua hiyo ya China itahusisha sehemu ya anga iliyo chini ya ulinzi wa kisiwa hicho. 

Ingawa hakukuwa na taarifa yoyote kutoka Beijing hadi sasa, lakini tangu Rais Tsai aingie madarakani mwaka 2016, China imeongeza shinikizo lake la kijeshi, kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya kisiwa hicho, inachoamini kuwa ni sehemu ya mamlaka yake inayotaka kujitenga. 

Endapo Lai atamrithi Tsai kwenye uchaguzi wa mwakani, uwezekano wa daktari huyo aliyesomea Harvard kuchukuwa hatua kali na za wazi zaidi kupingana na China ni mkubwa na hivyo pia uwezekano wa Beijing kuchukuwa njia iliyoitumia Hong Kong.

Vyanzo: Reuters, AFP, AP