1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa Biashara upunguze Umasikini

P.Martin22 Machi 2007

Hata ikiwa soko huru hupiga jeki ukuaji wa kiuchumi,ukuaji huo hauzalishi nafasi mpya za ajira wala haupunguzi umasikini.

https://p.dw.com/p/CHlO

Kwa hivyo ile dhana inayopigiwa debe kuhusu “Msaada wa Biashara” yapasa kufikiriwa upya ili umuhimu utolewe kupunguza umasikini,badala ya kuongeza tu biashara.

Katika mkutano uliofanywa juma lililopita katika mji mkuu wa Kenya Nairobi,Profesa wa uchumi Mohamed Ali Rashid,wa chuo kikuu cha Bangladesh–North South University,amesema kuna sababu nyingi sana za kutia mashakani uhusiano uliopo hivi sasa kati ya biashara wazi na ukuaji.Mkutano huo ulitayarishwa na CUTS-shirika lisilo la kiserikali likiwa na makao yake nchini India na ajenda kuu ilikuwa “Uhusiano kati ya Biashara, Maendeleo na Kupunguzwa kwa Umasikini”.

Kwa maoni ya Profesa Rashid,ni nchi chache sana zilizokua kiuchumi kwa kipindi kirefu,bila ya sehemu ya biashara ya kigeni kuongezeka katika pato la taifa.Ikiwa kuregezwa kwa masharti ya biashara kutasaidia kuongeza mahitaji ya ndani ya bidhaa zinazohitaji kutengenezwa na wafanyakazi, basi wafanyakazi zaidi watahitajiwa na mishahara pia huenda ikaongezeka.Lakini ikiwa wengi walio masikini hawana ujuzi wa kazi na wanaohitajiwa ni wafanyakazi wenye ujuzi,basi umasikini hautopunguka au huenda hata ukaongezeka.Kwa sababu hiyo ni muhimu kwa serikali kujishughuklisha zaidi na mikakati inayolenga kupiga vita umasikini ili wale walio masikini wapate nafuu fulani.Hiyo humaanisha kuwa serikali zinapaswa kuanzisha sera za kitaifa zitakazohakikisha kuwa wamasikini pia watanufaika na ukuaji wa biashara ya nje.

Wakati huo huo mradi wa Msaada wa Biashara,uliyozinduliwa Hong Kong mwaka 2005 kwenye mkutano wa Shirika la Biashara Duniani-WTO umekosolewa kwa sehemu fulani.Mpango huo ni chombo kinachotumiwa na nchi tajiri kupendekeza kuzisaidia nchi zilizo masikini na zile zinazoendelea,kuingia katika masoko ya kimataifa.

Lakini nchi zinazoendelea na hata zilizoendelea, zimethibitisha kuwa mara kwa mara,vipingamizi vya ndani,huzinyima nchi masikini nafasi ya kushiriki kikamilifu katika masoko hayo.Kwa sababu hiyo Profesa Rashid kutoka Bangladesh amesema,uwezo wa kujadiliana,wa nchi zinazoendelea na zenye maendeleo madogo sana,kuhusika na suala la biashara,wapasa kuimarishwa,ili makubaliano yanayopatikana katika majadiliano ya WTO yatie maanani maslahi ya wamasikini katika nchi hizo. Muhimu zaidi ni haja ya kuwasadikisha washirika wa kibiashara katika nchi zilizo tajiri,kuupanga upya mradi wa Msaada wa Biashara ili mpango huo kweli uwe chombo cha kupunguza umasikini.