1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msemaji mkuu wa Polisi Uganda auawa

17 Machi 2017

Afisa polisi kwa umaarufu nchini Uganda ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Kampala, katika tukio lililowashtua wengi na kumlaazimu rais Yoweri Museveni kuagiza kamera ziwekwe katika miji yote mikubwa.

https://p.dw.com/p/2ZRo7
Uganda - Polizisten getötet
Picha: Getty Images/AFP/G. Grilhot

Inspekta Jenarali Msaidizi wa Polisi Andrew Felix Kaweesi alihudumu kama msemaji wa jeshi la polisi na alikuwa mmoja wa maafisa wa juu kabisaa wa polisi katika taifa hilo. "Alipigwa risasi na kuuawa asubuhi hii wakati akiondoka nyumbani kwake kuja kazini," alisema Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi Kale Kayihura katika mazungumzo na shirika la habari la Ufaransa AFP.

"Kaweesi alikuwa na maafisa wawili wa polisi wanaomlinda ambao pia waliuawa. Lengo la mauaji hayo bado halijajulikana," aliongeza Kayihura.

Mauaji ya askari polisi ni jambo  nadra nchini Uganda, na mauaji hayo yanafanana na mauji ya afisa wa jeshi mwezi Novemba mwaka 2016 na mwendesha mashitaka mwandamizi mwezi Machi 2016.

Kundi kubwa la wakaazi lilikusanyika katika eneo la tukio ambako miili ya maafisa ilikuwa imeanguka katika gari jeusi, huku damu ikichuruzika katika vio vilivyopasukapasuka sambamba na gari hilo lililoharibiwa vibaya. Miili hiyo baadae iliondolewa.

Uganda - Polizisten getötet
Maafisa wa kitengo cha uchunguzi wa jinai cha polisi wakichunguza eneo la tukio alikouawa msemaji wa polisi ya Uganda Felix Kaweesi Machi 17, 2017. Nyuma ni gari alimokuwa.Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Mashuhuda wasimulia walichokiona

Mkaazi wa eneo hilo alielezea kuona wanaume wanne wakiwa kwenye pikipiki mbili wakishambulia gari walimokuwa wakisafiria maafisa hao wa polisi majira ya saa tatu na nusu asubuhi wakati wakielekea kazini.

"Walifyatua risasi za mfululizo kwa kutumia silaha zinazofanana na AK47," alisema Mohammad, dereva wa pikipiki maarufu Bodaboda, ambaye anaishi na kufanya kazi katika eneo hilo.

"Pikipiki hizo zilitokea nyuma wakati gari hilo likiondoka kutoka nyumbani kwa Kaweesi. Dereva wa gari alijaribu kuongeza mwendo lakini ziliipita gari hiyo na kuanza kuifyatulia risasi," alisema Mohammad mwenye umri wa miaka 30 ambaye alikataa kutaja jina lake la pili.

"Pikipiki hizo zilikuwa mpya na wauaji walikuwa walionekana kuwa weledi. Hawakuwa wamefunika nyuso lakini sikuweza kuona nyuso zao kwa sababu nilikimbia kuokoa maisha yangu."

Meya wa manispaa ya Kampala Charles Serunjoji alisema alikuwa "mvua ya risas -- risasi nyingi-- kutokea nyumbani kwangu karibu na eneo la tukio". "Siamini ninachokiona sasa. Nilimfahamu Kaweesi vizuri na nilikutana naye karibu wiki moja na nusu iliopita kuzungumzia kuiwekea lami barabara alikouawa," alisema.

Rais Museveni atoa maagizo

Rais Yoweri Museveni alilaani mauaji hayo na kuagiza kamera ziwekwe mara moja katika miji yote mikubwa nchini Uganda na kandoni mwa barabara kuu," ilisema ofisi yake katika taarifa.

Uganda Kristian Schmidt mit Felix Kaweesi
Marehemu Felix Kaweesi akiteta jambo na balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Uganda, Kristian Schmidt, wakati polisi ilipozingira nyumbani kwa kiongozi wa upinzani Dk. Kiiza Besigye baada ya uchaguzi wa 2016.Picha: DW/E. Lubega

Kaweesi alipata umaarufu baada ya kuongoza operesheni za polisi kuitikia maandamano makubwa ya vyama vya upinzani kufuatia uchaguzi mkuu uliokumbwa mwaka 2011.

Baada ya kuhudumu kwa muda kama kamanda wa polisi wa jiji la Kampala aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Operesheni na baadae mkuu wa dara ya rasilimali watu kabla ya kuteuliwa kuwa msemaji mkuu wa jeshi hilo Agosti 2016.

Alionekana mara kwa mara kwenye vituo vya televisheni, mara ya karibuni kabisaa ikiwa usiki wa Alhamisi kwenye runinga ya NTV, mmoja ya vituo vikubwa vya binafsi nchini humo.

Waliouawa kwa mtindo sawa

Mwezi Machi 2015 Joan Kagezi, mwendesha mashtaka mwandamizi alipigwa risasi barabani na muuaji akatoroka pamoja na mshirika wake kwenye pikipiki.

Novemba mwaka uliopita afisa wa jeshi la Uganda Meja Muhammad Kiggundu --- muasi wa zamani wa kundi la Allied Democratic Forces -- ADF -- alipigwa risasi na kuuawa akiwa katika gari lake na watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki mbili. Uhalifu wote huo bado haujatatuliwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Saumu Yusuf