1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

MSF:Mashambulizi ya raia yamefikia kiwango cha kutisha Sudan

Hawa Bihoga
13 Septemba 2023

Shirika la Madakari Wasio na Mipaka MSF limesema mashambulizi dhidi ya raia katika mji mkuu wa Sudan Khartoum, yamefikia kiwango cha kibaya tangu kuzuka kwa vita hivyo takriban miezi mitano iliopita.

https://p.dw.com/p/4WIWp
Wafanyakazi wa shirika la madaktari Wasio na mipaka wakiwa kwenye majukumu yao
Wafanyakazi wa shirika la madaktari Wasio na mipaka wakiwa kwenye majukumu yaoPicha: Patrick Bernard/abaca/picture alliance

Shirika hilo limesema takriban watu 49 waliuwawa, wengine zaidi ya 100 wakitibiwa majeraha makubwa na timu ya madaktari wa shirika hilo, huku kukiwa na taarifa za wahanga zaidi katika jiji hilo.

Mnamo siku ya Jumapili zaidi ya watu 43 waliuwawa baada ya mashambulizi ya anga ya kijeshi kusini mwa mji mkuu Khartoum.

Wakati siku ya Jumamosi takriban watu sita waliuwawakatika shambulio lililofanywa kwenye makazi ya raia, katika mikasa yote miwili watu kadhaa walijeruhiwa.

Nako katika mji wa Al-Fashir katika eneo la Darfur magharibi mwa nchi ambapo nako kwa kiwango kikubwa umeathirika na mapigano makali tangu kuzuka kwa mzozo, kati ya jeshi chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kikosi cha msaada wa dharura RSF kikiongozwa na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo, watu 4 waliuwawa na wengine 48 walijeruhiwa kwa milipuko na risasi.

Soma pia:Watu 30 wauwawa katika mashambulizi ya anga Sudan

Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa mataifa Volker Turk aliliambia Baraza la Haki za binadamu huko Geneva hapo jana Jumanne kwamba, wiki iliopita zaidi ya raia 103 waliuwawa wakati wa operesheni za kijeshi kwa pande zote mbili huko Khartoum na Omdurman.

Alisema mapema mwezi Septemba,Ofisi ya haki za binadamu Umoja wa Mataifa ilimepokea taarifa za kuaminika za matukio 45, yaliyohusisha wahanga wasiopungua 95.

Katika matukio hayo visa 75 viliwahusu wanawake, mwanamume mmoja na watoto 19.

"Hii inaonesha ni kiasi gani hali ni mbaya na kengele ya hatari."

Aliliambia baraza hilo na kuongeza kwamba matukio hayo yanaripotiwazaidi katika jimbo la Khartoum na maeneo ya Darfur na Kordofan.

Mashirika ya kiutu yataka viongozi wa dunia kuchukua hatua

Takriban watu 7,500 wameuawa nchini Sudan tangu mzozo huo ulipozuka Aprili 15, kulingana na makadirio ya wafuatiliaji wa mzozo huo.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na kiutu zaidi ya 50, wakiongozwa na Tirana Hassan, Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch wameitaka jumuiya ya kimataifa ishirikiane katika kutatua janga linaloendelea mbele ya uso wa dunia.

Kwa mujibu wa mashirika hayo watu milioni 20 sawa na asilimia 42 ya wasudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na watu milioni 6 miongoni wanakaribia baa la njaa.

Soma pia:Zaidi ya watu milioni 7 ni wakimbizi wa ndani Sudan kutokana na vita

Ripot yao imeendelea kuainisha kwamba takriban watoto 498 wamefariki kutokana na njaa, huku asilimia 80 ya hospitali na vituo vya afya vikikosa huduma za msingi.

Tangu Aprili, wakati mapigano ya wazi yalipoanza mjini Khartoum, zaidi ya watu milioni tano wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Juhudi za kidiplomasia nazo katika miezi ya mwanzoni mwa vita mara kdhaa zilishindwa kufikia lengo la usitishaji vita na ghasia huku hakuna dalili za kumalizika kwa mapigano.