1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji aliyewachukua watu mateka auawa Ufaransa

23 Machi 2018

Polisi nchini Ufaransa wamempiga risasi na kumuua mtuhumiwa aliyewashika mateka watu huko kusini mwa nchi hiyo. Waziri Mkuu wa Ufaransa Edouard Philippe amesema taarifa zote zinaashiria kuwa ni kitendo cha ugaidi.

https://p.dw.com/p/2urug
Frankreich Trebes - Polizeiaufgebot nahe Geiselnahme in Supermarkt
Picha: Reuters/R. Duvignau

Taarifa zinaeleza kwamba maafisa wa polisi wa nchini Ufaransa walivamia duka kubwa la kuuza biadhaa katika mji wa Trebes ambako mshambuliaji alikuwa amewachukua watu mateka na hatimaye walimuuwa mtu huyo kwa kumpiga risasi.

Takriban watu watatu wameuwawa kwenye shambulio hilo na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Polisi imesema mtu huyo aliuwawa muda mfupi tu baada ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza kuwa shambulio hilo linafanana kabisa kuwa ni la kigaidi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/F. Lenoir

Rais Macron ameyasema hayo akiwa mjini Brussels, Ubelgiji anakohudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.  Macron amesema yuko pamoja na wote wanaoshughulikia hali hiyo. Macron amesema anajiandaa kurejea nyumbani katika muda mchache ujao. Waziri mkuu wa Ufaransa bwana Edouard Philippe pia amesema shambulio hilo ni la kigaidi.

Mshambuliaji huyo anayeaminika kuwa ni raia wa Morocco ametajwa kuwa alikuwa anaitwa Redouane Lakdim. Mtu huyo alikuwa na mahusiano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS). kwa mujibu wa taarifa za polisi mshambuliaji huyo alikuwa kwenye orodha ya watu waliokuwa wanafuatiliwa na polisi baada ya kuhusika na mashambulio matatu katika mji wa Carcassone na karibu na mji wa Trebes. Mshambuliaji huyo katika madai yake kablya ya kuuwawa alitaka mmoja wa watuhumiwa katika mashambulio ya mjini Paris aachiwe huru. Mauaji hayo ya leo yametokea wakati ambapo Ufaransa bado katika hali ya tahadhari kubwa baada ya mashambulizi ya Kijihadi ya tangu mwaka 2015, pamoja na ya mwezi Januari mwaka huo wakati amabpo ofisi za gazeti la Charlie Hebdo zilishambuliwa na watu 12 walikufa.

Duka la Super U katika mji wa Trebes
Duka la Super U katika mji wa TrebesPicha: picture-alliance/dpa/Google

Waziri wa Mambo ya Ndani Gerard Collomb alipokuwa njiani kwenda kwenye eneo hilo, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba, eneo la kusini-magharibi mwa Ufaransa ambako leo Ijumaa kumetokea mashambulizi limeharibiwa kutokana na uchochezi wa makundi ya Kiislam yenye itikadi kali.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo