Mshirika wa Marcon ajitoa kwenye kinyang’anyiro cha umeya
14 Februari 2020Kujiondoa kwa Griveaux ni pigo kubwa kwa chama cha Rais Macron cha La Republique En Marche, ambacho kilitarajia kutumia nafasi hiyo ya heshima kubwa ya meya wa mji mkuu kujijengea msingi wenye nguvu kisiasa. Griveaux ameilaumu tovuti hiyo na mitandao ya kijamii kwa kuchapisha taarifa ambayo ameitaja kuwa ni mashambulio mabaya kabisa yanayolenga maisha yake binafsi.
Ameongeza kusema kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja, yeye na familia yake wamezongwa na tuhuma na matamshi ya uwongo, uvumi, mashambulio kutoka kwa watu wasiojulikana, kudukuliwa kwa mazungumzo yao binafsi kupitia kwenye baruapepe na hata kutolewa vitisho vya kuuawa.
Griveaux aliyasema hayo kwenye televisheni akisisitiza kwamba tangu kuchapishwa kwa video hiyo ya ngono siku ya Alhamisi anaona mambo yanazidi kuvuka mipaka na kwenda mbali zaidi.
Benjamin Griveaux alijiuzulu kutoka kwenye wadhifa wa uwaziri mdogo na msemaji wa serikali mnamo mwezi Machi mwaka jana ili kugombea umeya, na hadi sasa alikuwa hajapata uungwaji mkono wa kutosha. Matokeo ya kura ya maoni yalimuweka kwenye nafasi ya tatu nyuma ya wapinzani wake meya aliyeko madarakani kupitia chama cha Kisoshalisti, Anne Hidalgo, na mgombea wa chama cha kihafidhina, Rachida Dati.
Hatua ya Rais Macron ya kumchagua Griveaux kuwa mgombea wa nafasi hiyo ya meya wa jiji la Paris ilisababisha mivutano ndani ya chama cha En Marche, hasa baada ya kada wa juu wa chama hicho na mfuasi mkubwa wa Macron, Cedric Villani, alipotakiwa asigombee umeya ili amuachie Griveaux nafasi hiyo. Villani alikataa na matokeo yake akafukuzwa kwenye chama. Sasa, mtaalamu huyo wa hesabu yumo kwenye kinyang'anyiro hicho kama mgombea huru.
Rais Macron anatarajiwa kugombea tena urais mnamo mwaka 2022, na hivyo kwa chama chake kushinda umeya wa jiji la Paris lingekuwa ni jambo zuri kwake kisiasa, hasa kwa kuzingatia kwamba chama chake kinatarajiwa kupoteza kura katika maeneo ya vijijini, hali inayosababishwa na sera yake ya kazi, ambayo wengi wanaiona kama haiwatendei haki wanyonge.
Chanzo: https://p.dw.com/p/3XlTi