Mshukiwa wa mashambulio ya mabomu ya Madrid akamatwa Rabat
29 Januari 2008Raia wa Moroko anayetuhumiwa kuhusika katika mashambulio ya mabomu dhidi ya treni mjini Madrid nchini Uhispania mnamo tarehe 11 mwezi Machi mwaka wa 2004 amekamatwa mjini Rabat nchini Moroko.
Abdelilah Hriz, mwenye umri wa miaka 29, atashitakiwa nchini Moroko kwa kuhusika katika mashambulio hayo mabaya ya mabomu kuwahi kufanywa barani Ulaya, ambapo watu 191 waliuwawa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Moroko kukubali kumfungulia mashataka raia wake kwa uhalifu uliofanywa nje ya nchi hiyo.
Duru za mahakama nchini Moroko zinasema alama za vidole vilipatikana katika nyumba moja karibu na mjini Madrid ambamo vifaa vya kulipuka vilikuwa vikitengenezwa.
Mwezi Oktoba mwaka jana mahakama ya Uhispania iliwahukumu watu 21 waliopanga mashambulio ya mabomu mjini Madrid na kuwaondolea mashitaka wanaume wengine watatu.