1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msiba mkubwa Cambodia

Admin.WagnerD23 Novemba 2010

Jana (22 Novemba 2010), mtafaruku kwenye halaiki ya watu kwenye mji mkuu wa Phnom Penh, nchini Cambodia, ulisababisha mamia ya watu kupoteza maisha yao, huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya.

https://p.dw.com/p/QFtJ
Mtafaruku katika daraja la Mto Mekong nchini Cambodia hapo jana (22 Novemba 2010), ambapo zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha. (Picha ya AP/Heng Sinith)
Mtafaruku katika daraja la Mto Mekong nchini Cambodia hapo jana (22 Novemba 2010), ambapo zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha. (Picha ya AP/Heng Sinith)Picha: AP

Alfajiri ya leo (23 Novemba 2010) kwenye mji mkuu wa Cambodia, Phnom Penh, ving'ora vya magari ya uokozi vilienda sambamba na harakati za kupapia roho. Tayari zaidi ya watu 300 wameshapoteza maisha na bado vikosi vya uokozi na wasamaria wema wanaendelea kuzitambua maiti kadhaa zinazoelea chini ya daraja baina ya mto Mekong na Tonle Sap.

Haijulikani bado nini hasa kilichosababisha ajali hii ambayo Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hun Sen, ameitaja kama msiba mkubwa zaidi tangu kuporomoka kwa utawala wa kikatili wa Pol Pot hapo mwaka 1979, lakini inasemekana mmoja ya watu waliokuwa kwenye halaiki hiyo iliyokuwa ikishiriki Tamasha la Maji, alipiga kelele kwamba daraja lilikuwa linavunjika. Ndipo watu walipoghumiwa na kuanza kukimbia, kukanyagana na wengine kuchupa kwenye mto Mekong.

Fashifashi kwenye sherehe za Tamasha la Maji nchini Cambodia, ambalo safari hii (2010) limemalizika kwa msiba
Fashifashi kwenye sherehe za Tamasha la Maji nchini Cambodia, ambalo safari hii (2010) limemalizika kwa msibaPicha: AP

Miongoni mwa wahanga wa ajali hii ni vijana waliokuwa wanarudi nyumbani wakitoka kwenye muziki. Mfanyabiashara mmoja aliyekuwa karibu na eneo hilo anasema kwamba kiasi ya watu 1,000 walikuwepo kwenye daraja wakati ajali inatokea.

Waziri Mkuu Hun Sen ameliomba radhi taifa kwa ajali hii, akatangaza maombolezo ya kitaifa na ameteua tume ya kuchunguza mkasa mzima.

Kwenye hospitali hii ya taifa, bado mamia ya majeruhi wanaendelea kuletwa, wengi wao wakiwa ni wale waliounguwa kwa umeme baada ya kuamua kutokujirusha kwenye maji kama wenzao. Mmoja kati yao ni kijana wa miaka 23, ambaye anasema alikuwapo katikati ya halaiki wakati mtafaruku ulipoanza.

Jana ilikuwa ni siku ya mwisho ya Tamasha hili la Maji, ambayo ni sherehe kubwa na muhimu kwenye utamaduni wa Cambodia. Wakambodia hutumia sherehe hii kuushukuru Mto Mekong kwa kuwapa ardhi yenye rutuba na samaki. Katika siku za tamasha, kawaida mamia kwa maelfu ya Wakambodia hukusanyika hapa kucheza, kunywa na kuburudika. Lakini safari hii, sherehe imegeuka msiba.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Bernd Musch-Borowska/AFPE

Mhariri: Othman Miraj