Msichana wa miaka 16 kuhukumiwa Ujerumani
27 Januari 2017Mahakama katika mji wa Celle uliopo kaskazini mwa Ujerumani ilitarajiwa kutoa uamuzi wake siku ya Alhamisi. Safia alizaliwa mjini Hannover mnamo mwaka 2000, baba yake ni Mjerumani na mama yake anatokea Morocco. Wazazi hao walichana ambapo mama yao aliwalea wanawe kwa kuzingatia misingi ya dini ya kiislamu. Safia anakabiliwa na mashtaka ya kukusudia kuua, kujeruhi na pia kuunga mkono kundi la kigaidi, makosa ambayo mtu anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela hapa nchini Ujerumani.
Mwaka 2008 Safia alionekana katika mtandao wa Yotube akiwa anasoma Quran pamoja na muhubiri wa kundi la Salafisti Pierre Vogel ambaye baadae alionekana kumsifia mtoto huyo na kusema kuwa ni dada yao mdogo katika Uislamu wakati huo Safia alikuwa na umri wa miaka 7. Mwaka 2009 Pierre Vogel aliweka tena video kwenye mtandao huo akiwa na Safia ambaye alikuwa amevalia hijab.
Mwaka 2015 Safia alikuwa amerudi nyuma kimasomo na alizidi kuendelea na msimamo wake mkali, mwalimu wake alimfahamisha mwalimu mkuu wa shule baada ya kuiona video ya Safia na muhubiri wa Kisalafisti na vilevile walitoa taarifa kwa polisi na kuomba hatua zaidi za kiusalama zichukuliwe.
Mwezi wa Januari mwaka 2016 Safia alionekana katika uwanja wa ndege ambako alisafiri kwenda mjini Istanbul, Uturuki akiwa peke yake. Mama yake alimfuata Safia siku chache baadaye lakini baada ya kuvifahamisha vyombo vya usalama na hasa wasiwasi wake juu uwezekano wa mwanae kuingizwa katika makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali . Alifanikiwa kumrudsiha mwanawe huyo na uchunguzi ulianza mara moja kama vile kuchunguza mawasilainao ya simu na kumfuatilia mienendo yake.
Kifungo cha miaka sita
Mwendesha mashtaka hata hivyo amependekeza kifungo cha watoto cha miaka sita dhidi ya binti huyo wa miaka 16. Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wanasema wanaamini kwamba Safia alitumbukizwa katika mambo ya itikadi kali tangu akiwa mtoto na kwamba aliwafuata maafisa wa polisi kwa muda kwenye kituo cha treni katika mji wa kaskazini wa Hannover na wakati polisi walipomuita ili ajitambulishe ndipo Safia alipotoa kisu na kumjeruhi mmoja wao kwa kumdunga shingoni kabla ya kuzidiwa nguvu na polisi mwingine.
Katika kufunga malalamiko kwa upande wa serikali waendesha mashtaka pia wamemuomba jaji amuhukumu Mohamad Hassan mwenye umri wa miaka 20 kijana wa Kijerumani mwenye asili ya Syria kwa kushindwa kuwaarifu polisi shambulio alilolipanga Safia huku akiwa analijua. Takriban watu 900 wamesajiliwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS hapa nchini Ujerumani wengi wao ni wanawake na wengine ni watoto wenye umri kati ya miaka 13 na 14. Wanakwenda kupigana kwa niaba ya kundi hilo huko nchini Iraq na Syria.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/RTRE/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman