Msikiti Mwekundu wa Islamabad umevamiwa na wanajeshi wa serekali ya Pakistan
10 Julai 2007Wanafunzi wa kike na wa kiume wa Madrassa ilioko ndani ya masikiti huo wiki kadhaa kabla ya hapo walianzisha harakati za utumaiji nguvu, kama zile zilizokuwa zikitumiwa na Wataliban katika Afghanistan, kupinga vitendo vya umalaya na pia kuweko maduka yanayouza kaseti za Video za muziki, hivyo kukabiliana na nguvu za dola.
Naam, tena kuna tamati nyingine, lakini katika mtindo ule ule anaojuwa Jeneral Pervez Musharraf, mkuu wa Pakistan. Kati ya sifa alizokuwa nazo jenerali huyo ni kudhihirisha kwamba yeye ni mbabe aliyeazimia kikweli kukabilia na tatizo, kufa na kupona. Kuchukuwa muda mrefu katika kulitanzua tatizo ni kwenda kinyume na tabia ya wanajeshi.
Baada ya kuvamiwa Msikiti huo Mwekundu, na licha ya maombolezi kwa wale waliokufa na pia watu, angalau, kushusha pumzi kwamba vita hivyo vya neva vimemalizika, bado linabakia suali. Jee malumbano haya ya ajabu yalikuwa ni ya azima? Jee serekali isingeweza kutafuta njia nyingine katika wiki zote ambapo mzozo huu ulidumu? Vipi iliwezekana kwamba katikati ya mji mkuu wa Pakistan, licha ya tahadhari zote za kiusalama zilioko, Waislamu wenye siasa kali waliweza kukusanya silaha nyingi kama hizo? Na vipi inawezekana kwamba idara za usalama zinazotajwa zinajuwa kila kitu kinachotokea hazijaarifiwa kwamba wapiganaji wa kigeni waliopata mafunzo walijificha ndani ya msikiti huo?
Wakati wowote pale serekali ya Pakistan inapopambana na Waislamu wenye itikadi kali, kuna kama unduma kuwili, kwani bila ya kuunga mkono kwa nguvu kutoka upande wa serekali hiyo na idara zake za uslama, basi Wataliban na jamaa zao walio na itikadi kama zao wasingeweza kuwa kama walivyo sasa. Hapa dola ya Pakistan inapigana dhidiya matunda ya yale ilioyapanda hapo zamani- kama vile invovuna Marekani kile ilichopanda huko Iraq na Afghanistan. Haishangazi basi kwamba katika maeneo yenye watu wenye siasa kali kabisa, huko kaskazini magharibi ya Pakistan, ndipo leo kulifanywa maandamano makubwa dhidi ya Rais Musharraf.
Maoni mengi hadharani yanaonesha kwamba katika mkasa huu, huenda kwa mara ya kwanza katika harakati za aina hii, watu wengi wako nyuma ya serekali. Hali kama hiyo haijawa wakati Perevez Musharraf alipoiunga mkono Marekani baada ya mashambulio ya Septemba 11 huko Marekani au pale majeshi yake yalipofanya operesheni kubwa za kijeshi katika mkoa wa Waziristan ulioko karibu na mpaka wa Afghanistan. Mara hii sio watu wengi waliomlaumu Jenerali Musharraf na kusema kwamba kiongozi huyo anafanya haya kwa kufuata amri ya Marekani.
Kwamba mtindo wa maisha ya Kitaliban umetaka kujichomoza katikati ya jamii ya Pakistan ni jambo lililofanya tabaka nyingi ya jamii hiyo kujitenga na watu wenye siasa kali. Kumewekwa alama sasa. Lakini kuwawekea watu wenye siasa kali kikomo, haitoshi tu kuendesha operesheni za kijeshi. Yule ambaye anataka kuiondosha mizizi ya shule za Koran, basi mwishowe ni lazima awekeze zaidi katika shule za serekali. Na kwa upande wa siasa, mwishowe mwenendo wa demokrasia unahitajika kwa haraka kuweko huko Pakistan ili kuchomoze nguvu huru za kupambana na watu walio na siasa kali.