Msimu mpya wa ligi ya Ujerumani
5 Agosti 2011Msimu huu wa Bundesliga unaanza wakati timu mbalimbali zinahesabu hasara ya kuwakosa wachezaji wake kutokana na kuumia na majeraha waliopata kabla ya msimu kuanza na hivyo basi kuwalazimu kuwa nje katika mechi za kwanza za timu zao mbalimbali.
Ni kutokana na mechi za kirafiki na pia mashindano ya kuwania kombe la Ujerumani wiki iliyopita na vile vile fainali za Copa America ambazo zimewasababisha wachezaji mbalimbali kuchoka na kuumia jambo linalozusha swali kuhusu uwepo wa mechi nyingi za kimataifa.
Kiasi wachezaji 50 wanaocheza katika ligi ya Ujerumani Bundesliga wamesemakana kukosa kucheza katika mechi za ufunguzi wa msimu wikendi hii kutokana na maumivu waliyo nayo.
Tukianza na timu bingwa, Borrusia Dortmund ilikasirishwa wiki hii wakati ripoti za afya zilidhihirisha kuwa mchezaji wake raia wa Paraguay Lucas Barrios atakosa kiasi wiki tano au sita za kwanza za msimu baada ya kuumia katika fainali ya mashindano ya Copa America mwezi uliopita.
Kocha Jurgen Klopp alieleza kuwa athari kwa msuli wa Barrios ni kubwa tofauti na paraguaya ilivyoiambia timu hiyo bingwa Ujerumani. Ameeleza kuwa ni jambo la kuudhi na linatia dosari uhusiano kati yao na shirikisho la soka nchini Paraguay.
Ama kwa wachezaji wengine Jefferson Farfan na Caludio Pizzaro wanaoichezea timuya Schalke 04 na Werder Bremen pia wametengwa nje ya uwanja baada ya kuumia katika mechi za kuwadia mashindano hayo Copa America na kuwakosesha kushiriki mashindano hayo.
Timu mbalimbali za Ujerumani zimekasirishwa na kuuumia wachezaji kumia wakicheza katika mechi za kimataifa tukio ambalo linakumbukwa ni lile la mwaka uliopita la Arjen Robben aliuumiza msuli wake wa paja katika mashindnao ya kombe la dunia alipokuwa akiichezea Uholanzi.
Na hatimae timu ya Stuttgart ambayo iliepuka kwa tundu ya sindano kuingia katika eneo la hatari kwenye meza ya ligi hiyo msimu uliopita, itaikaribisha Shalke o4 hii leo bila ya mlinzi wake wa kiungo cha kati Goerg Niedermeier, aliyeumia paja na atakuwa nje kwa wiki sita zijazo, na pia Methieu Del Pierre ambaye atakuwa nje kwa miezi kadhaa kutokana pia na maumivu ya paja.
Sasa basi hapo kesho timu ya Bayern Munich inatarajiwa kuteremka kwa mara ya kwanza msimu huu dimbani dhidi ya Borrusia Monchengladbach uwanjani Munich.
Msimamo wa timu hiyo msimu huu ni kuiwinda Borussia Dortmund kama alivyosema rais wa Bayern, Uli Höness baada ya timu yake hiyo kutumia takriban euro milioni 41.3 msimu huu wa joto kukiimarisha kikosi hicho.
Matamshi ya Höness yanatokana na uhamisho na uekezaji wa kikosi chake katika kiungo cha ulinzi baada ya kupoteza magoli 40 msimu uliopita kwenye ligi hiyo.
Bayern ina mshirikisha kipa mpya anayetoka Schalke 04 manuel Neuer aliyetuzwa mchezaji bora wa mwaka na pia imemnunuwa mlinzi wa timu ya Uingereza Jerome Boateng.
Hawa miongoni mwa wachezaji wengine wapya, wanatazamiwa kuitoa sura na uwezo halisi wa Bayern Munich.
Mechi za kirafiki
Katika matayarisho ya Mashindano ya Kombe la dunia mwaka 2014, timu mwenyeji inacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu ya Argentina mwezi unaokuja Septemba kila mmoja akimakaribisha mwenzake. Hayo ni kwa mujibu wa shirikisho la soka nchini Brazil CBF.
Wapinzani hao wa jadi waliopata matokeo duni katika mashindano ya mwezi uliopita ya Copa America wakati wote walipotolewa katika robo fainali watakutana kwanza Argentina tarehe 14 Septemba huku mechi ya marudio ikitarajiwa kufanyika mjini Belem wiki mbili baadaye.
Kocha wa Brazil Mano Menezes amesema atatumia mechi hizo kuwakagua wachezaji ambao hawajawahi kushirikishwa awali kutokana na kuwa chaguo lake la kikosi cha kwanza kitacheza Ulaya.
Argentina kwa upande wake italitembelea bara la Asia na kucheza mechi dhidi ya Venezuela mjini Calcutta Septemba 2 na Nigeria mjini Dhaka siku nne baadaye.
Lakini kabla ya hapo timu hiyo mwenyeji wa mashindano ya kobe la dunia 2014 inatarajiwa kushiriki mechi ya kirafiki dhidi ya Ujerumani Agosti 10.
Na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löwe amewaita wachezaji wa kiungo cha kati ambao watashiriki kwa mara ya kwanza katika mechi ya kimataifa, kama vile Ilkay Gundogan, Marco Reus na wachezaji wengine 8 wa timu ya Bayern Munich katika kikosi kitakachoshuka dimbani wiki ijayo.
Mpambano huo utakuwa ni wa kwanza kati ya nchi hizo mbili tangu Juni 2005 wakati Brazil iliifunga wenyeji Ujerumani 3-2 katika nusu fainali ya mashindano ya kombe la Confederation linalohusisha mataifa bingwa ya mabara yote.
Ujerumani haijawahi kuifunga Brazil tangu ushindi wake wa mabao 2-1 mjini Cologne mnamo 1993.
Na katika mipambano 20 kati ya timu hizo mbili, Ujerumani imeshinda mara 3 pekee nakufanikiwa kutoka sare mara tano na kushindwa mara 12.
Ligi ya Uingereza
Msimu wa ligi ya Uingereza unaanza rasmi na timu jirani Manchester City na Manchester United zinateremka uwanjani hapo kesho huku City ikiwania kuikweza sifa yake dhidi ya mpinzani wake.
Manchester City ilishinda mwisho taji hilo la Uingereza mnamo mwaka 1968 mwaka ambao Mashetani wekundu Manchester united ilitawazwa kwa mara ya kwanza mabingwa barani Ulaya na tangu hapo imefanikiwa kujinyakulia mataji 12 ya ligi hiyo ya Uingereza yote chini ya ukufunzi wa sir Alex Ferguson.
Manchester City ambayo kwa wakati mmoja Ferguson alisema ni timu yenye fujo jingi, sasa pamoja na washindi wa pili msimu uliokwisha Chelsea ndiyo tishio kubwa kwa matumaini ya Manchester united kuendelea kulishikilia taji hilo.
Ferguson mwenyewe amekiri kwenye vyombo vya habari kuwa wanatarajia ushindani mkali kutoka timu hiyo pinzani jirani.
City ilionesha maendeleo kwa kumaliza katika nafasi ya tatu msimu uliokwisha. Ilihakikisha kuwa inaonesha mchezo mzuri katika ligi hiyo kando na mishahara mikubwa wanaolipwa wachezaji mahiri waliomo kwenye timu hiyo.
Mfungaji wa Argentina, Sergio Aguero ndiyo nyota ya hivi karibuni kusajiliwa kwenye timu hiyo kutoka timu ya Atletico Madrid katika kipindi cha uhamisho.
Chelsea kwa upande wake inaanza mwanzo mpya chini ya ukufunzi Andre Villas Boas.
Na hivi sasa ana kibarua kigumu kuhakikisha kuwa anapata matokeo mazuri kutoka kikosi cha wachezaji ambao baadhi wanaona wanazeeka.
Arsenal iliyotoka nafasi ya nne msimu uliokwisha imekuwa ikijitahidi kuwazuia wachezaji wake mahiri Cesc Fabregas na Samir Nasri baada ya Gael Clichy kujiunga na Manchester city.
Timu nyengine zinazotazamiwa kuwa kitisho msimu huu kwenye ligi hiyo ya Uingereza, ni Liverpool ambayo inajaribu kuirudisha sifa yake na kupambana msimu huu kulinyakuwa taji hilo tangu mwisho 1990.
Mwandishi: Maryam Abdalla
Mhariri:Abdul-Rahman