1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimu wa uhalifu Nairobi

1 Desemba 2013

Katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi kumekuwepo na ongezeko la uhalifu katika mwezi wa Novemba na mwanzoni mwa mwezi wa Disemba na kuanza kupungua mwezi wa Januari ambapo msimu huo unatambulika kuwa wa uhalifu Kenya.

https://p.dw.com/p/1AQW0
Nairobi mji mkuu wa Kenya.
Nairobi mji mkuu wa Kenya.Picha: picture-alliance/dpa

Patrick Richer mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya matangazo ya kibiashara ya Sydney maisha yake ni yale wanaoishi wataalamu wa kigeni,akiishi kwenye viunga vya Nairobi vya watu wa kipato cha juu wakizingukwa na kuta refu za ulinzi na kuwekwa kwa usalama wa saa 24.

Lakini hapo mwezi wa Novemba masahibu ya mwishoni mwa juma yakamkuta: genge la wanaume 10 walijipenyeza kwa kuvunja uzio wa nyuma ya nyumba,wakawafunga kamba walinzi wake na kuvamia nyumba yake alfajiri kwa kutaraji kujinyakulia kitita cha fedha taslimu,vito vya tahamani na vitu vyengine vya matumizi.Richer mwenye umri wa miaka 39 alipigwa risasi mara mbili na alifikishwa hospitali na mke wake.Alitangazwa kuwa amekufa mara tu baada ya kufikishwa hospitalini.Majambazi walioivamia nyumba yake walikuwa wamevalia sare za polisi na kwa mujibu wa repoti waliiba televisheni,komyuta za mkononi na simu.

Tukio hilo la kufadhaisha limekuja wakati kukiwa na mwendendo unaozidi kuwa mbaya katika mji mkuu wa Kenya Nairobi ambalo ni wimbi la uhalifu wa kabla ya kipindi cha Krismasi unaotekelezwa na wezi ambao kila kukicha wanazidi kuwa tayari kuuwa kukidhi haja zao.

Uhalifu wa msimu

Rocky Hitchcock mshauri wa usalama katika kampuni ya Ulinzi ya KK mojawapo ya kampuni kubwa binafsi za ulinzi mjini Nairobi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uhalifu huo wa msimu unajulikana na makampuni ya ulinzi kama ni " manunuzi ya Krismasi" ambapo ujambazi na kuteka nyara magari kunaongezeka dhidi ya wataalamu wa kigeni na Wakenya walio matajiri.

Nairobi mji mkuu wa Kenya.
Nairobi mji mkuu wa Kenya.Picha: Fotolia/Natalia Pushchina

Nairobi ambapo baada ya miaka imekuja kujipatia jina baya la "Nairobbery" ikimaanisha mji wenye majambazi wa kutumia nguvu ni miongoni wa miji yenye pengo kubwa kabisa kati ya matajiri na masikini duniani.

Matajiri huishi kwenye majumba makubwa ya kifahari wakilindwa na uzizo wa umeme,walinzi binafsi na mifumo ya elektroniki ya kutowa onyo wakati wa hatari. Takriban nyingi ya nyumba hizo huwa na milango na madirisha yenye kuwekwa vyuma na baadhi ina na vyumba vya usalama ikiwa kama sehemu ya mwisho ya kujihifadhi.

Lakini pia kuna vitongoji duni vilivyozagaa jijini na mamilioni ya watu wanishi kwenye vibanda na kukosa hata mahitaji ya msingi kabisa.Kila siku vijana wa kiume wa vitongoji hivyo huwa wanakwenda mijini au kwenye maeneo ya viwanda kutafuta kazi za vibaruwa.

Kitongoji duni cha Kibera kilioko Nairobi.
Kitongoji duni cha Kibera kilioko Nairobi.Picha: Reuters

Mageuzi ya polisi ni muhimu

Eneo mojawapo lenye kiwango kikubwa cha uhalifu ni la Karen, kitongoji cha matajiri kilioko kusini magharibi ya mjii mkuu ambapo kuna nyumba enzi ya ukoloni zilioko kwenye maeneo makubwa ya ardhi. Mtaa mzima wa nyumba hizo ulishambuliwa hivi karibuni isipokuwa ile ya Makamo wa Rais William Ruto ambapo nyumba yake hulindwa na kikosi maalum cha polisi.Pia kumekuwepo na ongezeko la wizi wa udokozi madukani na chakula nchini kote.

Ziada ya hayo duru za usalama zinasema askari wa usalama waliostaafu na wale walioko kazini wamekuwa wakizidi kujihusisha na uhalifu.Polisi mwenye kulipwa wa mshahara wa chini kabisa hupokea chini ya dola 200 kwa mwezi.

Polisi wa kutuliza fujo katika mji wa Nairobi.
Polisi wa kutuliza fujo katika mji wa Nairobi.Picha: Reuters

Mageuzi ya polisi ilikuwa mojawapo ya nguzo za msingi katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010 baada ya kubainika kwamba zaidi ya watu 1,000 waliuwawa na wengine walikuwa wahanga wa ukatili wa polisi kutokana na machafuko ya uchaguzi wa mwaka 2007 uliozusha utata.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu