1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msukumo wa utengano Cameroon watokana na wanaoishi ughaibuni

Oumilkheir Hamidou
26 Oktoba 2017

Vuguvugu la wanaopigania kujitenga eneo la Cameroon linazungumza Kingereza linapata nguvu katika nchi hiyo. Lakini kutokana na ukosefu wa viongozi wenye haiba katika eneo hilo, msukumo unatokana na wanaoishi ughaibuni

https://p.dw.com/p/2mYHQ
Demonstration Kamrun Unabhängigkeit für anglophone Regionen
Picha: Reuters/J.Kouam

Vuguvugu la wanaopigania kujitenga eneo la Cameroon linazungumza kiengereza linapata nguvu katika nchi hiyo ya Afrika magharibi. Lakini kutokana na ukosefu wa viongozi wenye haiba katika eneo hilo, msukumo unatokana na wanaoishi ughaibuni. Hayo lakini ni kwa mujibu wa wachambuzi.

Oktoba mosi iliyopita wanaharakati wanaopigania kujitenga eneo hilo- majimbo mawili ya Cameroon ambako wakaazi wake wanazungumza Kiingereza , eneo wanaloliita , Ambazonia, walipelekea Rais Paul Biya kuamuru vikosi vya usalama kuingilia kati-tukio lilosababisha dazeni ya watu kuuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Machafuko hayo yaliyozuka mwishoni mwa mwaka 2016 na kutishia kugeuka "uasi kwa mtutu wa bunduki" kwa mujibu wa shirika la kimataifa linaepusha mizozo kutokea-ICG, yalichochewa kwanza na jopo la mashirika ya kiraia- CACSC mashuhuri kwa jina "The Consortium".

Picha iliyochukuliwa kutoka kwenye video inayoonesha maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia katika mji wa Buea
Picha iliyochukuliwa kutoka kwenye video inayoonesha maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia katika mji wa BueaPicha: Reuters/TV

Mgawanyiko kulingana na utawala wa zamani wa Ufaransa na Uingereza

Likiundwa Desemba mwaka 2016, jopo hilo linaloongozwa na Felix Khongo Agbor Balla linayaleta pamoja mashirika manne ya mawakili,  na vyama kadhaa vinavyopigania masilahi ya waalimu, linafuata msimamo wa wastani na kuunga mkono mshikamano pamoja na serikali kuu inayodhibitiwa kwa sehemu kubwa na wenye kuzungumza kifaransa.

Mwezi januari jopo hilo likavunjika na viongozi wake wawili wakakamatwa.Waliachiwa huru baadae lakini wengine kadhaa wakakimbilia nchi za nje ambako msimamo wa kisiasa ukazidi makali na kujiunga na wale wanaopigania kujitenga.

Ufaransa na Uingereza waliligawa koloni hilo la zamani la Ujerumani lililokuwa chini ya usimamizi wa jumuia ya mataifa baada ya vita vikuu vya kwanza vya dunia. Mwaka mmoja baada ya ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na ufaransa kupata uhuru mwaka 1961, sehemu ya kusini ya eneo la Cameroon lililokuwa chini ya utawala wa ukoloni wa uingereza ikajiunga na mfumo wa shirikisho uliobadilishwa miaka 11 baadae na kuwa "Jamhuri ya Muungano".

Katika maeneo ya kusini magharibi na kaskazini magharibi, wanakoishi karibu asili mia 20 ya wakaazi milioni 23 wa Cameroon, mapambano ya kujitenga yanasimamiwa na vikundi vya wenyeji wanaoendesha harakati zao kichini chini.

Waandamanaji wa Cameroon wakiwa nje ya hoteli alikokaa rais Paul Biya wakati alipohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa New York
Waandamanaji wa Cameroon wakiwa nje ya hoteli alikokaa rais Paul Biya wakati alipohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa New YorkPicha: picture alliance/AP Photo/B. Matthews

Muungano wa jopo la kusini la Ambazonia

Katika wakati ambapo tofauti zingalipo kuhusu mkakati na mbinu, makundi madogo maadogo ya wanaopigania kujitenga yamepaza sauti hivi kariibuni na kuhimiza matumizi ya nguvu na sio tuu dhidi ya vikosi vya usalama bali pia dhidi ya raia wanaozungumza kifaransa.

"Bado mapambano makubwa ya kisiasa hayajaanza kuchochewa kutoka nje kutoka kwa wale wanaojitokeza hadharani na kudai uhuru wa  eneo la wanaozungumza kiengereza la Ambazonia" anasema Nguini Owona,mtaalam wa mikakati ya kijeografia kutoka eneo la Afrika kati.

Julius Ayuk Tabe Sisiku anaeishi Marekani ndie aliyejitangaza kuwa rais wa Ambazonia.Mtaalam huyo wa computa hajajulikani sana nchini Cameroon lakini anautumia mtandao wake wa kijamii wa Facebook kuwapatia mwongozo wafuasi wake. Anajaribu pia kutafuta uungaji mkono wa jumuia ya kimataifa kwa kile anachokipigania. Wanachama wengine wawili wa jopo hilo wanaoishi uhamishoni wametangaza kuunda jopo lao wanaloliita "Muungano wa jopo la kusini la Ambazonia- linalopigania pia uhuru na kutoa mwongozo wa namna ya kupambana dhidi ya serikali ya mjini Yaounde.

Wanaaopigania kujitenga eneo hilo wana miliki pia kituo cha televisheni ambacho ingawa kimepigwa marufuku nchini Ccameroon lakini kinarusha matangazo yake kutoka Afrika Kusini.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AFP

Mhariri: Gakuba, Daniel