1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chapo aahidi kuimarisha umoja baada ya machafuko ya Msumbiji

15 Januari 2025

Rais mpya wa Msumbiji, Daniel Chapo, ameapishwa Jumatano mbele ya hadhara ya viongozi waliolindwa vikali katika mji mkuu wa Maputo, kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya vurugu kupinga matokeo ya uchaguzi yenye utata.

https://p.dw.com/p/4pAAm
Msumbiji | Kuapishwa kwa Rais Daniel Chapo
Daniel Chapo (Kulia) akiapishwa kuwa Rais wa Msumbiji wakati wa sherehe ya iliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Maputo, Januari 15, 2025.Picha: Phill Magakoe/AFP

Chapo, mwenye umri wa miaka 48, anaendeleza utawala wa miaka 50 wa chama cha Frelimo katika taifa hilo la Afrika lenye utajiri wa gesi, huku kukiwa na madai kutoka kwa mpinzani wake Venancio Mondlane kwamba uchaguzi ulihujumiwa, hali iliyochochea machafuko ambayo shirika moja lisilo la kiserikali linasema yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300.

Wakati akiapishwa, Chapo aliapa kutumia nguvu zake zote "kutetea, kukuza na kuimarisha umoja wa kitaifa, haki za binadamu, demokrasia, na ustawi wa wananchi wa Msumbiji."

Hata hivyo, usiku wa kuamkia kuapishwa kwake, Mondlane alitishia "kusimamisha" serikali mpya kwa maandamano ya kila siku kufuatia wito wake wa awali wa mgomo wa kitaifa kabla ya sherehe hiyo. Mondlane, mwenye umri wa miaka 50 na anayependwa na vijana, anasisitiza kuwa uchaguzi wa Oktoba 9 ulipangwa kuipa ushindi Frelimo, ambayo imekuwa madarakani tangu Msumbiji ilipopata uhuru kutoka Ureno mwaka 1975.

"Utawala huu hautaki amani," Mondlane alisema katika hotuba yake kwenye Facebook Jumanne, akiongeza kuwa timu yake ya mawasiliano ilishambuliwa kwa risasi mitaani wiki hii. "Tutapinga kila siku. Ikiwa itamaanisha kusimamisha nchi kwa kipindi chote cha utawala huu, tutafanya hivyo."

Mzozo waongezeka Msumbiji kabla ya kuapishwa kwa Chapo

Wito wa kushirikiana kuendeleza nchi

Chapo alitoa wito wa utulivu Jumatatu, akiwambia waandishi wa habari katika bunge la taifa, "tunaweza kuendelea kufanya kazi na kwa pamoja, kwa umoja... kuendeleza nchi yetu."

Waangalizi wa kimataifa walisema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro, huku ujumbe wa EU ukilaani kile walichokiita "upotoshaji usio na sababu wa matokeo ya uchaguzi." Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alihudhuria kuapishwa huko, huku Ureno, iliyokuwa koloni la Msumbiji, ikimtuma Waziri wa Mambo ya Nje, Paulo Rangel.

Soma pia: Msumbiji yawapisha wabunge wapya kukiwa na hali ya utulivu

Kabla ya sherehe hiyo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na usalama kutoka Maputo, Johann Smith, aliiambia AFP kuwa kutokuwepo kwa idadi kubwa ya viongozi wa mataifa ya kigeni "kunatoa ujumbe mzito." Smith alisema, "Hata kutoka mtazamo wa kikanda, kuna kusitasita kukubali au kutambua ushindi wa Chapo."

Vikosi vya usalama vilifunga barabara katika maeneo yote ya Maputo na kuzunguka Uwanja wa Uhuru, ambako sherehe ya kuapishwa ilifanyika. Kiwango cha machafuko baada ya kuapishwa "kinategemea jinsi Chapo atakavyoshughulikia mgogoro huu," mchambuzi Borges Nhamirre aliambia AFP.

Hali ya utulivu yatawala licha ya vitisho vya Mondlane

Sherehe ya kuapishwa kwa wabunge Jumatatu ilifanyika kwa utulivu kiasi. Barabara zilikuwa tupu Jumatatu, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa ama kwa ajili ya kupinga sherehe hiyo au kwa hofu ya vurugu, wakati polisi wa kijeshi wakizunguka jengo la bunge na polisi wakifunga barabara kuu.

Hata hivyo, watu wasiopungua sita waliuawa katika maeneo ya Inhambane na Zambezia kaskazini mwa mji mkuu, kulingana na shirika la kiraia la Plataforma Decide.

Kiongozi wa upinzani Msumbiji arejea kutoka uhamishoni

Machafuko tangu uchaguzi huo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300, kulingana na takwimu za shirika hilo, huku vikosi vya usalama vikilaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Polisi pia wamethibitisha vifo vya maafisa wao.

Chapo, ambaye anatarajiwa kutangaza serikali yake mpya wiki hii, anaweza kutoa nafasi za uwaziri kwa wanachama wa upinzani kama njia ya kupunguza machafuko, alisema Eric Morier-Genoud, profesa wa historia ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Queen's Belfast.

Pia, kumekuwa na wito wa kufanyika kwa mazungumzo, lakini Mondlane amewekwa kando katika mazungumzo ambayo Chapo na rais anayemaliza muda wake, Filipe Nyusi, walifungua na viongozi wa vyama vikuu vya siasa.

Soma pia: Malawi yakabiliwa na mgogoro wa wakimbizi kutoka Msumbiji

Hata hivyo, Chapo amesema mara kwa mara kwamba yuko tayari kumjumuisha Mondlane katika mazungumzo. Mondlane, ambaye alirejea Msumbiji wiki iliyopita baada ya kujificha nje ya nchi kufuatia mauaji ya wakili wake mnamo Oktoba 19, amesema yuko tayari kwa mazungumzo. "Niko hapa kwa mwili wangu kusema kwamba ikiwa mnataka mazungumzo... niko tayari," alisema.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Chapo alipata asilimia 65 ya kura za urais, ikilinganishwa na asilimia 24 za Mondlane. Hata hivyo, kiongozi huyo wa upinzani anadai alipata asilimia 53 na kwamba taasisi za uchaguzi za Msumbiji zilichezea matokeo hayo.

Wabunge wa Frelimo pia wanatawala bunge lenye viti 250, wakiwa na viti 171 ikilinganishwa na viti 43 vya chama cha Podemos.