Mswada wa kupinga sheria ya afya waondolewa
25 Machi 2017Akizungumza na waandishi habari akiwa mjini Washington, Ryan amesema wamekosa kura za kutosha za kuitengua sheria ya afya ya Obamacare, na hivyo itabaki kuwepo kwa muda usiojulikana.
Rais Trump amewalaumu Wademocrat kwa kushindwa huko ingawa baadhi ya sehemu za sheria hiyo zina matatizo, lakini bado inafanya kazi vizuri na imeweza kupunguza idadi ya watu wasio na bima ya afya nchini Marekani kwa kiasi kikubwa.
Trump alitumia nguvu zake zote za kisiasa kusogeza mbele mswada huo. Alitumia siku kadhaa kuwashawishi Warepublican wenzake waliokuwa wakionyesha ukaidi. Baadae Trump alisema kuwa amekatishwa tamaa na wala hajashangazwa sana na kushindwa kwa mswada huo wa kuiondoa sheria ya afya ya Obamacare.
Mvutano huo ulikuwa ni tukio la kumfungua macho Trump, mfanyabiashara bilionea aliyeingia Ikulu ya Marekani ya White House bila ya uzoefu wa kisiasa wala uelewa wa taratibu za kiserikali, ikiwemo diplomasia inayohitaji kulishawishi bunge.
Kushindwa kwa msaada huo ni jaribio la pili la kubadilisha sera la rais huyo mpya, ambaye alishuhudia pendekezo lake la kuziwekea marufuku ya kusafiri ya muda baadhi ya nchi za Kiislamu likipingwa mara mbili tofautui na mahakama za nchi.
Rais Trump alikutana na spika wa bunge, Paul Ryan, mapema jana na baadae kuzungumza naye kwa njia ya simu baada ya kudhihirika wazi kuwa chama cha Republican hakijaweza kupata kura za kutosha kupitishwa mswada huo.
"Nilimwambia la kufanya pekee ni kuiahirisha kura ya mswada huo na akakubaliana nami katika uamuzi huo", amesema Paul Ryan spika wa bunge la Marekani. Lakini wakati Trump alipokuwa akiwalaumu wabunge wa upande Democrat kwa kutoupigia hata kura moja mpango wake huo, Ryan alikubali kushindwa.
Trump akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa, alisema kuwa bado ana matumaini ya kwamba maafisa wake wataweza kuwasilisha sheria ya huduma ya afya bora zaidi.
Kufuatia kushindwa kwa jitihada za Trump za kutaka kuitengua sheria ya Afya iliyowekwa na mtangulizi wake Barack Obama, baadhi ya Wamerekani walishusha pumzi na wengine walichanganyikiwa huku wote wakijua kuwa mjadala wa kitaifa juu ya bima ya afya bado haujamalizika.
Kuahirishwa kwa mswada huo wa kura dhidi ya bima ya afya ya Obamacare iliyochochewa na wanachama wa chama cha Republican, kumedhihirisha kuwa mgawanyiko uliopo ndani ya bunge la Marekani utaendelea kuwepo.
Taarifa zilivyozidi kusambaa, Wamarekani waligawanyika katika kambi tofauti. Kuna kambi iliyofurahia kuona jitihada za Wademokrat zimefanikiwa, na kambi iliyopata shauku kwa kutegemea kuwa Warepublican watakusanyika tena na kujaribu kutimiza ahadi zao za kuitengua sheria ya afya ya Obamacare.
Kufuatia taarifa hiyo, msanii kutoka Michigan Marekani, Alysa Diebolt mwenye umri wa miaka 27, ameandika katika ukurasa wa Facebook na kusema amefurahi kuwa watu anaowajua wanaotumia bima ya afya ya bei nafuu ya Obamacare hawatoipoteza. "Nimefurahi, nadhani kitu kizuri," amesema Alysa Diebolt.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dpae/afp
Mhariri: Caro Robi