1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtambo wa umeme wa nyuklia nchini Iran wafungwa kwa dharura

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
21 Juni 2021

Mtambo wa umeme wa nyuklia wa Bushehr nchini Iran wafungwa kwa sababu za kiufundi na kutokana na hali hiyo maafisa wametoa tahadhari juu ya uwezekano wa kukosekana umeme wakati matengenezo yanapoendelea kufanyika.

https://p.dw.com/p/3vH19
Iran Atomkraftwerk in Bushehr
Picha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Televisheni ya taifa ilitangaza juu ya kufungwa kwa kiwanda pekee cha umeme wa nyuklia nchini Iran hapo jana Jumapili. Ni mara ya kwanza Iran kuripoti juu ya kufungwa kwa dharura kituo hicho cha umeme wa nyuklia cha Bushehr. Msemaji wa kampuni ya umeme ya taifa, Tavanir, Gholamali Rakhshanimehr, amesema mtambo huo wa Bushehr utaendelea kufungwa kwa muda wa siku tatu hadi nne akitarajia kuwa masuala hayo ya kiufundi yatakuwa yametatuliwa.

Soma zaidi:Rais wa Iran autetea mkataba wa nyuklia

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, japokwa msemaji huyo wa kampuni ya Tavanir hakutoa maelezo zaidi lakini inaaminika kuwa masuala ya kiufundi yanahusiana na kukosekana kwa vipuri vya kurekebisha hitilafu iliyojitokeza. Mtambo wa nyuklia wa Bushehr ambao ni mradi wa pamoja baina ya Iran na Urusi umekuwa unakabiliwa na matatizo mnamo miezi ya hivi karibuni. Na hasa tangu kuanza kwa mdororo wa uchumi uliosababishwa na vikwazo vilivyowekwa na Marekani. Pamekuwapo na taarifa za mara kwa mara kwamba Iran haina uwezo wa kununua vipuri kutoka Urusi.

Mtambo wa nyuklia wa Bushehr ni mradi wa pamoja kati ya Iran na Urusi
Mtambo wa nyuklia wa Bushehr ni mradi wa pamoja kati ya Iran na UrusiPicha: Getty Images/IIPA

Mataifa makubwa ya dunia yanauvumilia mtambo huo wa nyuklia wa Bushehr kwa sababu unatumika kwa madhumuni ya amani. Madini ya Urani kwa ajili ya mradi huo wa nyuklia yanatoka Urusi na unasimamiwa na shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, IAEA. Ujenzi wa mtambo huo uliopo kwenye mji wa bandari wa kusini wa Bushehr ulianza mnamo miaka ya 70. Ulikamilika baadaye kwa msaada wa Urusi na kuanza kufanya kazi mnamo mwaka 2011.

Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia, madini ya urani yanayotumika kwenye mtambo wa Bushehr yanarutubishwa nchini Urusi. Iran pia inawajibika kurudisha Urusi mabaki ya urani iliyotumika. Kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani nchi hiyo hairuhusiwi kununua vifaa na vipuri kutoka Urusi.

Soma zaidi:IAEA ina wasiwasi kuhusu vinu vya nyuklia vya Iran

Mtambo huo wa Bushehr wa megawati 1000 za kuzalisha umeme wa nyuklia, uliibua wasiwasi katika eneo la kanda ya mashariki ya kati kwa sababu upo kwenye eneo linalokumbwa na mitetemeko ya ardhi. Kufungwa kwa kiwanda hicho kumetokea wakati Iran na nchi zenye nguvu kiuchumi duniani zinajaribu kufufua makubaliano ya mwaka 2015 juu ya mpango wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo ya mjini Vienna, Austria ambayo mwakilishi wa Umoja wa Ulaya kwenye majadiliano hayo amedokeza kuwa wanakaribia kufikikia makubaliano.

Mwanamama ameshikilia picha ya rais mpya wa Iran aliyechaguliwa hivi karibuni Ebrahim Raisi
Mwanamama ameshikilia picha ya rais mpya wa Iran aliyechaguliwa hivi karibuni Ebrahim Raisi Picha: Atta Kenare/Getty Images/AFP

Hata hivyo mwakilishi wa Iran katika mazungumzo hayo mjini Vienna amesema Iran inataka dhamana kutoka kwa serikali ya sasa ya Marekani kwamba haitafuata nyayo za utawala wa rais wa zamani Donald Trump.

Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbass Araqchi, ambaye aliongoza ujumbe wa kidiplomasia wa Iran kwenye mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na mataifa yaliyobaki kwenye makubaliano hayo ya mpango wa nyuklia wa Iran (JCPOA) ambayo ni Urusi, China, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza aliyasema hayo mara baada ya kumalizika duru ya sita ya mazungumzo ya Vienna hapo jana jioni.

Vyanzo:DPA/AFP/https://p.dw.com/p/3vG4a