1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtandao wa jamii zana ya kutatua mizozo

27 Juni 2015

Wajumbe kutoka vyombo vya habari,taasisi za kisiasa na mashirika yasio ya kiserikali wamejadili uwezo wa mtandao wa jamii kuwa zana hai ya kuwahusisha wanawake katika mchakato wa kuzuwiya na kusuluhisha mizozo.

https://p.dw.com/p/1Fo7o
Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini Bonn
Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini Bonn.Picha: DW/N. Wojcik

Azimio la kihistoria nambari 1325 lililopotishwa na kikao cha nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa miaka 15 linaagiza hivyo na hiyo ilikuwa mada moto wakati wa warsha ya hivi karibuni ya Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya habari lililoandaliwa na Deutsche Welle mjini Bonn.

Leila Nachawati Rego mwanzilishi mwenza wa jukwaa la mtandao wa kijamii lililo huru la SyriaUntold mwenye maskani yake Madrid Uhispania anasema mtandao wa kijamii huwawezesha wanawake kuhadithia habari zao wenyewe ambazo zinahusu jamii ya kiraia na kuwa karibu na watu walioko mashinani bila ya habari hizo kuchujwa kisiasa.

Hata hivyo Sopheap Chak Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binaadamu nchini Cambodia anasema kuna mgawanyiko wa kijinsia katika fani ya teknolojia ya habari na mawasiliano na anatowa mfano wa kuwepo kwa washiriki wachache wa kike kwenye mtandao. Akizungumza kutoka Phnom Penh katika ujumbe aliotuma kwa video kwenye kongamano hilo amesema ni suala la dunia kwamba wanawake bado wanakabiliwa na ubaguzi unaofanyika chini ya misingi ya kijinsia.

Kauli za chuki

Katika suala la vurugu dhidi ya wanawake zinazofanywa kwenye mitandao Nachawati ametaja kwamba asilimia 95 ya kauli za chuki kwenye mitandao ziko dhidi ya wanawake.Anaona mawasiliano kwa kutojitambulisha na matumizi ya hati maalum za mtandao ni muhimu kwa wanawake wanaotumia mitandao ya kijamii kwani wanaweza kujihifadhi wenyewe.

Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini Bonn
Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini BonnPicha: DW/M. Müller

Ametowa kauli hiyo katika jopo la mjadala lililoendeshwa na Jaafar Abdul-Karim mwandishi wa habari na mwendesha kipindi cha mazungumzo cha Deutsche Welle na mtetezi wa kamati ya Ujerumani ya Wanawake katika Umoja wa Mataifa ya HeForShe.

Changamoto nyengine ambayo imetajwa na Wagaki Wasichnewski afisa wa Habari kwa Wananchi na Kituo cha Habari cha Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kupambana na Kuenea kwa Jangwa mjini Bonn ni ile ya kuwepo kwa kiwango cha chini cha kujuwa kusoma na kuandika kwa wanawake watu wazima katika maeneo ya vijijini.Yeye anasisitiza kutumia zana za zamani za kutowa habari kama vile radio ya vijijini pia ni muhimu.

Utatuzi wa mizozo

Ama Beatrice Frey Meneja wa Mitandao ya Kijamii katika Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa mjini New York anasema mitandao ya kijamii inaweza kuwa zana yenye guvu kuleta mwamko,kuandaa na kuipanga jamii na anasisitiza kwamba ingawa haiwezi kutatuwa mizozo lakini ikitumika ipasavyo inaweza kuwa zana moja miongoni mwa nyengine katika kusaidia utatuzi wa mizozo.

Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini Bonn
Jukwaa la Vyombo vya Habari 2015 mjini BonnPicha: DW/N. Wojcik

Naye makamo wa rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii barani Ulaya yenye makao yake mjini Brussels mchango wake katika warsha hiyo ya Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya habari ni kutaka kutumiwa kwa mambo yote mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vilivyozoelekea yaani vya kawaida ili kuwahusisha wanawake katika mchakato wa kutatuwa mizozo.Morrice aliukamilisha mdahalo huo kwa kusema ufumbuzi ni kutumia sauti zao wanatakiwa wasimame kidete na kuvunjilia mbali milango ya kuingilia kwenye majukwaa yote.

Warsha hiyo imeandaliwa kwa niaba ya mtandao Gender@international Bonn, Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani GIZ, Deutsche Welle,mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Bonn na Kamati ya Taifa ya Wanawake ya Ujerumani kwa Umoja wa Mataifa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/DW

Mhariri : Iddi Ssessanga