1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: unyanyasaji dhidi ya watoto umeongezeka

30 Desemba 2019

Ripoti ya shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto la UNICEF inasema Yemen, Afghanistan na Syria kuwa ni mataifa yenye mazingira magumu zaidi kwa watoto.

https://p.dw.com/p/3VUDS
Jordanien Mafraq Flüchtlingslager
Picha: picture-alliance/Xinhua/M. Abu Ghosh

Mustakabali wa watoto uko kwenye mashaka. Shirika la UNICEF linasema kuwa kumekuwa na ongezeko mara tatu zaidi la mashambulizi kwa watoto hasa katika maeneo yenye kushuhudia vita katika muda wa muongo mmoja uliopita.

Mnamo mwaka 2018 Umoja wa Mataifa ulinakili zaidi ya visa 24,000 vya ukiukaji wa haki za watoto, idadi hiyo ikiwa ni mara tatu zaidi ya mwaka 2010. Katika nusu ya visa hivyo, watoto wengi waliuawa kwa mashambulizi ya roketi za angani huku wengine wakiuawa kwa kukanyaga mabomu ya ardhini.


"Migogoro na vita duniani vimeongeza na vinadumu kwa muda mrefu na kusababisha umwagikaji wa damu. Watoto ndio wenye kuathirika zaidi," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la UNICEF Henrietta Fore.

Mizozo katika mataifa ya bara Arabu hasa Syria na Yemen imesababisha ongezeko la watoto kuwa wakimbizi huku takwimu zikionyesha kuwa zaidi ya watoto milioni 2.5 wanaishi kama wakimbizi nje ya Syria.

Kadhalika, takriban watoto milioni 1.2 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa kibinadamu kutokana na vita vilivyotokea nchini humo yapata miaka sita iliyopita.

Mataifa ya vita yaliyoathirika zaidi

Aidha Syria, Yemen, Afghanistan, Libya, Mali, Nigeria, Myanmar, Somalia na Sudan Kusini ndiyo mataifa yaliyotajwa kuwa miongoni mwa mataifa yenye mazingira magumu zaidi kwa watoto.

Armut in Afghanistan -  Kinderarbeit
Kamra, 10, akifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza matofali nje ya mji wa Kabul, Afghanistan.Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Watoto wengi wanaoishi katika mataifa hayo wanadhulumiwa, wananyanyaswa, wanasafirishwa kwa ajili ya kutumiwa kwa biashara ya ngono na kufanyishwa kazi kama watumwa, wanasajiliwa kama wapiganaji wa waasi miongoni mwa mateso mengine.

Kando na migogoro na vita, kuibuka kwa maradhi na majanga ya kimazingira pia yameathiri maisha ya watoto. Ugonjwa wa surua na Ebola hasa katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo umeathiri zaidi watoto kutokana na ugumu wa kusafirisha misaada katika eneo hilo.

Si hayo tu, mabadiliko ya tabia nchi pia yametajwa kuathiri maisha ya watoto duniani. Unicef inasema kuwa zaidi ya watoto nusu bilioni wanaishi katika sehemu ambazo zina uwezekano mkubwa wa kushuhudia mafuriko huku takriban watoto milioni 160 wakiishi katika sehemu kame. 

Kwa sasa, Shirika la UNICEF linawatolea wito viongozi na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kuungana ili kumaliza ukiukaji wa haki za watoto duniani. 


 Vyanzo: (DPA/UNICEF)