1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa Ghaddafi, Seif Al Islam sasa kuwania urais wa Libya

3 Desemba 2021

Mahakama nchini Libya imepitisha uamuzi wa kumruhusu Seif Al Islam, kugombea urais na baada ya kupindua aumuzi wa tume ya taifa ya uchaguzi wa kumuondowa kwenye orodha ya wagombea Urais kwa madai ya kutokidhi vigezo.

https://p.dw.com/p/43nq8
Lybien Saif al-Islam Gaddafi, Sohn des libyschen Führers Muammar Gaddafi
Picha: Mast Irham/dpa/picture alliance

Mahakama nchini Libya imepitisha uamuzi wa kumruhusu Seif Al Islam, mwanawe Moammar Ghaddafi, kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao na hivyo kuupindua uamuzi uliokuwa umechukuliwa na tume ya taifa ya uchaguzi wa kumuondowa kwenye orodha ya wagombea Urais kwa madai ya kutokidhi vigezo.

Hatua hiyo ya mahakama ya mkoa wa Kusini wa Sabha, ilitangazwa jana Alhamisi baada ya Seif al-Islam kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa wiki iliyopita wa tume kuu ya uchaguzi nchini Libya, kumuondoa katika orodha ya wagombea kwa kumtuhumu makosa ya zamani yanayohusiana na kutumia mabavu dhidi ya waandamanaji.

Mahakama imetoa nafasi ya kumfanya Seif Al Islam kuwa mgombea urais.

Libyen Sebha | Saif al-Islam al-Gaddafi registriert sich als Präsidenstchaftskandidat
Mgombea Seif Al Islam akitia saini fomu ya kugombea uraisPicha: Khaled Al-Zaidy/REUTERS

Hatua hii ya mahakama inampa nafasi kugombea uraisi katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 24 mwezi huu wa Disemba. Kwa takriban wiki moja, mahakama haikuweza kusikiliza rufaa hiyo baada ya watu wenye silaha  kuzingira eneo la mahakama na kuwazuia majaji kuingia katika jengo hilo.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Al Islam aliwashukuru majaji kwa kuhatarisha usalama wao akisema wamefanya hivyo ``kusimamia ukweli.'' Pia aliishukuru familia yake na wafuasi wake. Uchaguzi huo unakuja baada ya miaka mingi ya majaribio yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa kutafuta mustakabali wa kidemokrasia na zaidi sana kumaliza vita vya wenyewe nchini humo.

Kiini cha machafuko ya Libya yaliodumu kwa muongo mmoja sasa.

Libya imekumbwa na machafuko tangu kutokea kwa maandamano yaliyoungwa mkono na NATO na yaliompindua Moammar Gadhafi mwaka 2011. Katika muongo mmoja uliopita, taifa hilo lenye utajiri wa mafuta lilikuwa limegawanyika kati ya serikali mbili, moja ya mashariki inayoungwa mkono na kamanda mwenye nguvu Khalifa Haftar, na nyengine inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya huko mjini Tripoli, zote zikisaidiwa na vikosi vya kigeni kutoka Uturuki, Urusi na Syria na hata mamlaka tofauti za kikanda.

Mwaka 2015, Seif al-Islam alihukumiwa kifo na mahakama ya mjini Tripoli katika kwa kutumia vurugu dhidi ya waandamanaji katika vurugu za mwaka 2011 dhidi ya baba yake, ingawa uamuzi huo uliwahi kutajwa na mamlaka hasimu ya Libya. Al Islam anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Uchaguzi ujao unakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na migogoro kuhusu sheria zinazosimamia uchaguzi, migogoro ya hapa na pale kati ya makundi yenye silaha. Vikwazo vingine ni pamoja na mpasuko wa kina uliopo kati ya mashariki na magharibi ya nchi na uwepo wa maelfu ya wapiganaji wa ndani na hata wa kigeni.

Mwandishi: Bakari Ubena/APE

Mhariri:Yusuf Saumu