Mtoto wa Kipalestina auawa Ukingo wa Magharibi
31 Julai 2015Ni tukio ambalo Israel inalitaja kuwa ni la kigaidi, huku Palestina ikisema serikali ya Israel inahusika moja kwa moja na mauaji hayo ya kikatili. Matamshi hayo ambayo ni nadra na laana kutoka kwa viongozi wa Israel, wakitanguliwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu, hayakuwatia moyo Wapalestina. Badala yake, viongozi wa Palestina wanasema serikali ya Netanyahu inabeba dhamana jumla ya kuuliwa mtoto mchanga huyo na kukitaja kisa hicho kuwa ni "matokeo ya moja kwa moja ya miongo kadhaa ya kufumbiwa macho na serikali ya Israel, visa vya kigaidi vinavyofanywa na walowezi".
Maandamano yanatarajiwa kuitishwa baada ya sala ya Ijumaa katika maeneo yote ya Wapalestina. Wafuasi wa Hamas walioko madarakani Gaza wameitisha "Siku ya Ghadhabu" dhidi ya mashambulizi na uchokozi wa Israel.
Kwa miaka sasa, wanaharakati wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Israel au walowezi wamekuwa wakifanya visa vya uchokozi na ushari dhidi ya Wapalestina na Waisrael wenye asili ya Kiarabu, dhidi ya maeneo ya ibada ya Waislamu na Wakristo na hata dhidi ya wanajeshi wa Israel. Lakini vituko vingi kati ya hivyo havikuchukuliwa hatua ta kisheria na serikali ya Israel.
Netanyahu: "Kitendo cha kigaidi"
Alfajiri ya Ijumaa, kwa mujibu wa maafisa wa usalama wa Palestina, walowezi wanne wa Kiyahudi walizitia moto nyumba mbili zilizoko karibu na mji wa Douma, kaskazini ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Waliandika maneno ukutani kabla ya kutoroka kuelekea katika mtaa wa Wayahudi wa Maale Ephraim. Mojawapo ya maneno hayo yanamtakia maisha marefu Mesia.
Mtoto mchanga huyo, Ali Dawabcheh, aliyekuwa na umri wa miezi 18, ametiwa moto yu hai hadi kufa. Mama yake, Eham, mwenye umri wa miaka 26 na baba yake Saad na nduguye Ahmed mwenye umri wa miaka 4 wamejeruhiwa na kupelekwa katika hospitali moja ya Israel.
Hali ya mama mtoto ni mbaya sana, daktari mmoja wa Israel amesema na kuongeza "maisha yake yako hatarini. Baba mtoto pia ameunguwa kwa asilimia 80.
Msemaji wa jeshi la Israel amesema jeshi linafanya uchunguzi kujua waasisi wa shambulio hilo wamekimbilia wapi. "Ni kitendo cha kigaidi" amesema waziri mkuu Benjamin Netanyahu, huku waziri wake wa ulinzi, Moshé Yaalon, akikilaani pia na kukitaja kuwa kitendo cha kigaidi.
Watuhumiwa kufikishwa mahakamani
Saeb Erakat, mtu wa pili katika uongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, amesema: "Watu hawawezi kutenganisha shambulio hilo la kinyama na serikali inayowakilisha muungano kwa ajili ya ulowezi na ubaguzi wa rangi na mtengano." Yaariv Oppenheimer wa vuguvugu linalopigania amani amesema "mashambulio ya walowezi yamegeuka maradhi ya kuambukiza."
Akizungumza kupitia Radio Israel, Oppenheimer amekosoa "kufumbiwa macho na serikali visa vya matumizi ya nguvu dhidi ya wapalastina pamoja na hotuba za chuki."
Waziri Mkuu Netanyahu amewaamuru wanajeshi wa usalama watumie kila njia iliyoko kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
Kama kawaida ya kila siku ya Ijumaa, polisi wa Israel wamejazana katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina ikiwa ni pamoja na pembezoni mwa Harami Sharif unakokutikana msikiti wa Al Aqsa kuzuwia maandamano yanayopangwa kufanyika baada ya sala ya ijumaa.
Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef