1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe ajitokeza hadharani

17 Novemba 2017

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ameonekana kwa mara ya kwanza leo hadharani tangu jeshi lilipomuweka chini ya kifungo cha nyumbani wiki hii

https://p.dw.com/p/2npQT
Simbabwe Robert Mugabe hält Rede an der Uni
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Kujitokeza kwa Mugabe katika mahafali ya chuo kikuu, kumekuja wakati msururu wa mazungumzo ya dharura yakiendelea na viongozi wa kikanda kuhusu kuondoka kwake baada ya kuwa madarakani kwa miaka 37.

Jeshi la Zimbabwe linapata ugumu wa kuonyesha heshima kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 kwa kumuita rais na kamanda mkuu wa jeshi.

Lakini baadhi ya viongoziwa chama tawala ZANU-PF wanakosa subira na Mugabe, huku matawi mbalimbali ya chama hicho yakielezea kutokuwa na Imani naye katika mikoa ya Mashonaland Mashariki na Manicaland.

Bunge linatarajiwa kuanza tena vikao vyake Jumatano. Kuna uwezekano kuwa ZANU-PF huenda kikatumia utaratibu wa chama kumuwondoa Mugabe kwa kuungwa mkono na wabunge wa upinzani. Kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani Morgan Tsvangirai anasema Mugabe lazima ajiuzulu akiongeza kuwa mapambano ya kisiasa kati yake na Mugabe hayakuwa ya kiadui

Chris Mutsvangwa, mwenyekiti wa chama chenye ushawishi cha maveterani wa kivita nchini Zimbabwe amewaambia wanahabari kuwa Mugabe ameomba kupewa muda wa siku au miezi kadhaa Zaidi.

Mutsvangwa, mshirika wa makamu wa rais aliyetimuliwa hivi karibuni Emmerson Mnangagwa ambaye anatarajiwa kuongoza serikali mpya, amesema kuwa kati ya leo na kesho, watamuonya Mugabe kuwa mambo yake yamekwisha. Veteran huyo pia amesema mawaziri watatu wamekamatwa katika juhudi za jeshi kuwalenga washirika wa Mugabe. Waziri wa elimu Jonathan Moyo, waziri wa serikali za mitaa Saviour Kasukuwere na waziri wa fedha Ignatious Chombo wamewekwa jela pamoja na wengine. Habari hizo hata hivyo habari hizo hazikuweza kuthibitishwa maramoja.

Sherehe ya leo ya chuo kikuu ilionekana kumuewesha Mugabe kuonyesha sura ya uongozi, hata wakati miito ya kuondoka kwake ikiongezeka. Mugabe hakutoa hotuba kwenye sherehe hiyo, isipokuwa tu kusema kuwa kuwa sasa imefunguliwa rasmi na akapigiwa makofi baada ya kujiunga na umati katika kuimba wimbo wa taifa.

Taarifa ya jeshi iliyochapishwa na gazeti la seirkali la Herald na shirika la utangazaji la Zimbabwe imesema kuwa viongozi wake wanashauriana na Kamanda Mkuu wa jeshi Rais Robert Mugabe kuhusu njia bora ya kusonga mbele na litalifahamisha taifa baadaye kuhusu matokeo hayo haraka iwezekanavyo.

Jeshi linawatafuta maafisa wakuu ambao wamekuwa washirika wa mke wa rais, Bi Grace Mugabe, sehemu ya kundi linalofahamika kama G40 kwa sababu wengi wao wako katika miaka ya 40 na 50. Ni wa kizazi tofauti na kile kilichipigania uhuru kutoka kwa utawala wa wazungu.

Kamati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC imependekeza kuandaliwa mkutano wa kilele wa dharura kujadili hali hiyo. Haijafahamika wazi ni lini utaandaliwa.

Wakati huo huo, Rais wa Botswana Ian Khama amesema Mugabe anapaswa kusitisha juhudi zake za kusalia madarakani kwa sababu hana uungwaji mkono wa kidiplomasia kikanda wa kusalia madarakani.

Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Yusuf Saumu