Mugabe na Tsvangirai wafikia muafaka kugawana madaraka
12 Septemba 2008Hiyo ni baada ya juhudi za Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki aliyekuwa msuluhishi wa Umoja wa nchi za SADC katika mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe, na mtu ambaye hapo kabla alikuwa akilaumiwa kwa diplomasia ya kimya kimya.Hata hivyo makubaliano hayo yatawekwa hadharani Jumatatu ijayo.
Rais Mbeki ambaye alikuwa msuluhishi katika mzozo huo,pia alisema kuwa, viongozi hao wawili watatangaza serikali ya umoja wa kitaifa siku hiyo ya Jumatatu , na kutoa tumaini la kumalizwa kwa mkwamo mkubwa wa kiuchumi uliyopeleka madhila makubwa kwa wananchi wa Zimbabwe.
´´Makubaliano yamefikiwa kwenye maeneo yote ya ajenda zilizowasilishwa kwenye majadiliano.Kutakuwa na sherehe rasmi za utiaji saini siku ya jumatatu saa nne asubuhi hapa Harare ambapo nyaraka za makubaliano hayo zitasainiwa na viongozi wa Zimbabwe na kutolewa kwa wananchi.Nyaraka zote zimekwishasainiwa leo usiku, lakini zitasainiwa hadharani jumatatu´´.
Rais Mbeki ameelezea matumaini yake kuwa viongozi hao wawili wamethamiria kutekeleza yote yaliyokubaliwa , baada ya miezi miwili ya majadiliano kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu ambao unaelezewa ulitekwa nyara na utawala wa Rais Mugabe.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo mkuu Morgan Tsvangirai aliongoza dhidi ya Mugabe lakini chini ya 50 asilimia ya kura na hivyo kulazimisha uchaguzi huo kuingia katika duru ya pili ambayo ilisusiwa na upinzani kwa kile ilichosema kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi yao.
Viongozi kutoka sehemu mbali mbali dunia wamepongeza hatua hiyo iliyofikiwa jana na viongozi hao ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema makubaliano hayo yatakuwa kwa faida ya wananchi wa Zimbabwe waliyotaabika kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Rais wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC Jacob Zuma alimpongeza Rais Mbeki ambaye ni hasimu wake ndani ya chama hicho kwa kufanikisha kufikiwa kwa muafaka huo.
Mapema shirika la utangazaji la Afrika Kusini liliarifu ya kwamba katika makubaliano hayo Rais Mugabe ataongoza baraza la mawaziri ambapo Morgan Tsvangirai ataongoza baraza jipya la mawaziri litakaloundwa, yaani kutakuwa na mabaraza mawili ya mawaziri yatakayosimamia uendeshaji wa serikali na utekelezaji wa sera za serikali mpya ya mseto.
Kwa upande mwengine taarifa zilizovuja kutoka ndani ya chumba cha majadiliano ziliarifu ya kwamba viongozi hao wamekubaliana kuwa Rais Mugabe atadhibiti jeshi la nchi hiyo ambapo Morgan Tsvangirai ataongoza serikali pamoja na jeshi la polisi
Aidha Seneta David Coltart kutoka chama kidogo kilichojitenga na MDC alidokeza ya kwamba katika makubaliano hayo chama cha MDC kitakuwa na idadi ndogo ya mawaziri katika serikali ambapo kitakuwa na mawaziri 13 huku chama cha Rais Mugabe cha ZANU PF kitakuwa na mawaziri 15 na chama kilichojitenga na MDC kitakuwa na mawaziri watatu.
Hata hivyo nchi za magharibi zimepokea kwa tahadhari makubaliano hayo zikisema ya kwamba zitaiunga mkono serikali hiyo mpya ya mseto iwapo itampa madaraka zaidi Morgan Tsvangirai.
Umoja Ulaya umesema kuwa unasubiri kuona muundo wa serikali hiyo kabla ya kuamua upya juu ya vikwazo ilivyoiwekea Zimbabwe.
Lakini msemaji wa chama cha MDC Nelson Chamisa alisema kuwa makubaliano hayo ni kwa faida ya Zimbabwe na si kwa vyama vya kisiasa, na kuwataka wananchi wa nchi hiyo kuyaunga mkono.
►◄