1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mursi akutana na majaji

26 Novemba 2012

Rais Mohammed Mursi wa Misri anakutana na majaji baada ya mageuzi aliyoyafanya na kujipa madaraka zaidi, huku tayari athari za mgogoro huo wa kisiasa zikianza kuonekana kwenye uchumi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/16plx
Rais Mohammed Mursi wa Misri.
Rais Mohammed Mursi wa Misri.Picha: AP

Rais Mursi amefikia uamuzi huo kufuatia mgomo wa majaji pamoja na vyombo mbalimbali vya sheria nchini humo kugoma kufanya kazi hadi hapo atakapotengua maamuzi yake.

Baraza Kuu la Sheria nchini humo limesema kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Rais Mursi yafanye kazi tu katika masuala ya mamlaka likisema kuwa hatua hiyo haijakiuka azimio na hivyo kuwataka majaji ambao baadhi wameanza mgomo tangu jana kurejea kazini.

Ofisi ya rais nchini humo imekuwa ikirudia mara kwa mara kuwa na kuwahakikishia wananchi kuwa mageuzi hayo ni ya muda mfupi tu na kwamba kiongozi huyo anataka kufanya mazungumzo na makundi ya kisiasa kwa ajili ya kupata maelewano juu ya nini kiwepo kwenye katiba ya Misri. Suala la katiba ni moja ya mada kuu nchini humo na ndio kiini cha mzozo ulioibuka sasa.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Cairo, Hassan Nafaa, anasema ameziona juhudi za Mursi na majaji katika kuutatuta mzozo huo lakini akaongeza kuwa "hazieleweki". Nafaa anasema kuwa wanakoelekea ni kubaya zaidi na kwamba mambo yanazidi kuvurugika.

Huduma za kisheria zakwama

Licha ya Mursi kuchukua baadhi ya mamlaka za kisheria kuzusha maandamano makubwa nchini humo kama yale yaliyouondoa utawala wa zamani, kilio cha kukosekana kwa huduma za kisheria kimeanza kusikika.

Maandamano dhidi ya uamuzi wa Mursi mjini Cairo.
Maandamano dhidi ya uamuzi wa Mursi mjini Cairo.Picha: Getty Images/AFP

"Niliambiwa kuwa kesi ya mwanangu itasikilizwa leo. Nimekuja asubuhi hii lakini hakuna aliyefika. Si mwanangu si majaji. Mwanangu anashikiliwa na polisi, na hii mahakama haifanyi kazi leo hivyo ataendelea kubakia jela. Hii si haki kabisa." Alisema raia mmoja nje ya mahakama ya Cairo.

Pamoja na hayo, soko la hisa nchini humo limeshuka thamani kwa asilimia 10 hapo jana katika siku ya kwanza ya ufunguzi tangu kutangazwa kwa mabadiliko hayo na Rais Mursi.

Watu wengi nchini humo wanautazama uamuzi wa Mursi kujiongezea madaraka na kupunguza nguvu za vyombo vya sheria kuwa ni wa kidikteta. Raia wana hofu kuwa huenda Chama cha Udugu wa Kiilsamu cha Rais Mursi kina nia ya kuwarejesha walikotoka enzi za rais wa zamani Hosni Mubarak.

Zaidi ya watu 500 wamejeruhiwa katika mapambano baina ya polisi na waandamanaji na mtu mmoja amepoteza maisha. Picha za waandamanaji wakipambana na polisi wa kuzuia ghasia pamoja na miripuko ya mabomu ya machozi zimeenea katika uwanja wa Tahrir ambao ni kiini cha kumbukumbu ya vuguvugu lililopita la kuutoa madarakani utawala wa Mubarak.

Wanaharakati wameweka kambi katika uwanja huo kwa siku ya tatu mfululizo wakiweka vizuizi barabarani na hivyo kusababisha msongamano wa magari

Mwandishi: Stumai George/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef