1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mursi asaini rasimu ya Katiba

26 Desemba 2012

Rais wa Misri Mohamed Mursi ametia saini rasimu ya katiba kuwa sheria akisema hatua hiyo itasaidia katika kuumaliza mvutano wa kisiasa na kumruhusu kuangazia hatua ya kuirekebisha hali tete ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/1794p
Rais Mursi asaini katiba
Rais Mursi asaini katibaPicha: AP

Wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mgogoro wa kiuchumi umewakumba Wamisri katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita huku wengi wakikimbilia kuziondoa fedha zao kutoka mabenki ya taifa hilo na upande mwingine serikali ikiweka vikwazo vipya vya kuwakataza watu kuzipeleka nchi za nje fedha zao.

Matokeo juu ya kura ya maoni kuhusu katiba yaliyotangazwa Jumanne yameonyesha kwamba asilimia 63.8 ya wamisri wameiridhia katiba hiyo kwa kupiga kura ya ndio na kufungua njia ya kufanyika uchaguzi wa bunge katika kipindi cha takriban miezi 2 ijayo.

Asilimia 63.8 wapitisha katiba mpya
Asilimia 63.8 wapitisha katiba mpyaPicha: AP

Ni Ushindi wa nani?

Ushindi huo unamaanisha kundi la udugu wa kiislamu limepata ushindi wa tatu tangu alipoondolewa kwa nguvu madarakani kiongozi wa zamani Hosni Mubarak mwaka 2011 baada ya huko nyuma kushinda uchaguzi wa bunge na rais.

Ofisi ya rais Mursi imetangaza kwamba Jumanne usiku kiongozi huyo aliamua kutia saini kuwa sheria rasimu hiyo ya katiba ya tangazo rasmi la matokeo ya kura ya maoni yaliyoonyesha kwamba asilimia kubwa ya wamisri wameikubali katiba hiyo ambayo ni ya kwanza tangu kutimuliwa madarakani Hosni Mubarak.

Urbi et Orbi Segen 2012
Picha: dapd

Mgawanyiko miongoni mwa wamisri

Hata hivyo pamoja na kutajwa kwamba wengi wameiridhia katiba hiyo,kumejitokeza mgawanyiko mkubwa katika nchi hiyo ya kiarabu hali ambayo imekuwa ikizusha maandamano ya ghasia mara kwa mara katika mitaa ya mji mkuu Cairo.Makundi ya upinzani yanailaani katiba hiyo yakisema kwamba imezingatia zaidi misingi ya itikadi kali na haifuati misingi ya kidemokrasia.Wapinzani wanalalamika kwamba katiba hiyo inatoa nafasi kwa viongozi wa kidini kuingilia kati hatua za kuunda sehria na kuyaacha kando makundi ya waliowachache bila ulinzi wa kisheria.

Hata hivyo rais Mursi aliyesaidiwa na kuungwa mkono kuingia madarakani na washirika wake katika kundi la udugu wa kiislamu anaamini kupitishwa katiba hiyo ni hatua muhimu kabisa ya kumaliza kipindi cha mvutano na hali ya wasiwasi wa kiuchumi ambayo imelikumba taifa hilo.

Ametilia mkazo kwamba katiba hiyo mpya inatoa ulinzi kwa kila mwananchi wa Misri bila ya kujali makundi yao akisema kwamba wamisri wamechoshwa na maandamano ya mitaani ambayo yamesababisha kuzuia hali ya kawaida kurejea pamoja na kuizuia serikali kutoangazia suala la uchumi.

Uchumi wayumbayumba

Kwa hivi sasa serikali imechukua sheria ya kudhibiti fedha kwa kuwazuia watu kutosafirisha nje au kuingiza nchini zaidi ya dola 10,000,hii ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kuukabili mgogoro wa kiuchumi ambao umeanza kuzusha mashaka nchini humo.

Ägypten Proteste in Alexandria
Picha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images)

Serikali ya rais Mursi inadai kwamba wapinzani wanauharibu uchumi wa nchi kwa kurefusha mvutano wa kisiasa.Hata hivyo kinachoshuhudiwa kwa sasa katika mitaa ya mjini Cairo kitovu cha maandamano ni utulivu huku yakionekana makundi ya watu wachache tu wanaoandamana na kuchoma matairi wakati wa usiku

Aidha Mursi na serikali yake wameahidi kuanzisha hatua isiyopendwa na wengi ya kuongeza kiwango cha kodi pamoja na kupunguza bajeti ya matumizi ya nchi ili kupata mkopo kutoka shirika la fedha la kimataifa IMF. Rais huyo pia anatarajiwa kwenda Ujerumani Januari 29 kuomba msaada wa kuujenga upya uchumi wa taifa lake.

Mwandishi :Saumu Yusuf

Mhariri:Sekione Kitojo