Mursi ataka bunge kufunguliwa tena
9 Julai 2012Baada ya takribani wiki moja madarakani, hatua ya Rais Mursi ya kutaka bunge likutane licha ya mahakama kusema kwamba bunge hilo sio halali, inatishia kuyumbisha utulivu wa Misri na kusababisha vurugu miezi 17 baada ya kuondolewa kwa nguvu madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.
Jeshi liliungana na hatua ya mahakama ya kikatiba kuvunja bunge ili kujipa madaraka ya kutunga sheria nchini Misri. Mahakama hiyo ilisema ilichukua uamuzi huo kwa kuwa thuluthi moja ya bunge hilo ilichaguliwa kwa njia isiyo halali. Hatua hii ilikikasirisha chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kilikuwa na wajumbe wengi katika bunge hilo.
Mursi aitisha uchaguzi wa bunge
Mwanaharakati mmoja ambaye pia ni wakili maarufu nchini Misri, Negad Borai, amesema hatua hii inaonekana kuanzisha mzozano ambao umekuwa ukichemka kwa miezi mingi. Kwa sasa jeshi halina nguvu kamili ya kupambana na rais aliyechaguliwa.
Kulingana na shirika la habari nchini humo, jeshi hilo linasemekana kukutana kwa kikao cha dharura ili kujadili hatua hiyo ya Mursi. Pia mahakama kuu ya katiba iliyofutilia mbali bunge la nchi hiyo mwezi uliopita inatarajiwa kukutana hii leo kuzungumzia uamuzi wa Rais Mohammed Mursi.
Mursi ambaye ni kutoka chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kimekuwa katika hali ya kutoelewana na jeshi, pia ameitisha uchaguzi wa bunge kufanyika katika siku 60 zijazo ili kuweza kupata katiba mpya ya nchi hiyo inayotarajiwa kuundwa mwishoni mwa mwaka huu.
El-Baradei atoa onyo
Hatua hizi mbili za Mursi zinaonekana kuwa muhimu sana kwa kiongozi ambaye alitiliwa shaka na baraza la jeshi lililokuwa linaongoza Misri kushinda uchaguzi katika duru ya pili iliyofanyika tarehe 16 na 17 ya mwezi uliopita.
Hata hivyo katika maagizo yake Mursi hakutaja chochote juu ya mahakama ya kikatiba, na inatiliwa shaka iwapo rais huyo ana haki kisheria kwenda kinyume na maagizo ya mahakama.
Mohamed El-Baradei ambaye ni mwanaharakati wa mageuzi na pia mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ameonya kuwa hatua ya Mursi huenda ikatishia kudhalilisha nguvu za mahakama nchini humo.
Agizo la Mursi kutaka bunge kufunguliwa tena limekuja saa chache baada ya kukutana na maafisa wakuu wa Marekani mjini Cairo waliowasilisha ujumbe wao kwa rais huyo uliotoka moja kwa moja kwa Rais Barrack Obama kumuhakikishia kuwa Marekani itakuwa na ushirikiano mzuri na Misri.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP
Mhariri: Mohammed Khelef