Mursi kujaribu kutuliza munkari
29 Novemba 2012Hotuba ya Mursi inakuja wakati baraza la kutunga katiba likijiandaa kupiga kura leo kuhusu muswada wa katiba mpya ambayo Mursi anatumai itamaliza mgogoro unaoendelea hivi sasa. Baraza lililopewa jukumu la kuandika katiba mpya limemaliza kazi yake mapema leo na muswada wa katiba hiyo utapigia kura baadae hii leo. Lakini wakati wapinzani wa Mursi wanaendelea na maandamano yao ya wiki nzima katika uwanja wa tahrir mjini Cairo, wakosoaji wanasema jitihada za baraza la katiba kuharakisha mchakato wa kuandika katiba hiyo zinaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Watu wawili wameuawa na mamia kujeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika nchini Misri kote.
Udugu wa Kiislamu wacheza kamari
Chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho ndicho kilichomsimamisha Mursi katika uchaguzi wa mwezi Juni, kinatumaini kuwa tangazo la kikatiba lililotolewa na rais litafutwa na katiba mpya ambayo itaidhinishwa kupitia kura ya maoni. Hii ni kamari inayochezwa na chama hiki kutokana na imani yake kwamba kinaweza kuhamasisha wapiga kura wa kutosha na kushinda katika kura hiyo ya maoni. Chama hicho kimeshinda chaguzi zote tangu Hosni Mubarak alipoondolewa madarakani.
Maafisa kutoka chama cha Udugu wa Kiilsamu wamesema Mursi ataeleza katika hotuba yake leo, sababu za yeye kutoa tamko hilo la kikatiba na kuorodhesha alizoona kuwa ni njama zilizokuwa zinapangwa na wapinzani wake, hasa waliyo na uhusiano na utawala uliyopita. Walisema rais huyo wa kwanza kuchaguliwa na umma nchini Misri, atatoa wito wa kuwepo na umoja wa kitaifa.
Maandamano ya kumuunga mkono Mursi
Chama cha Udugu wa Kiislamu na washirika wake wameitisha maandamano siku ya Jumamosi katika uwanja wa Tahrir, jambo linalotishia kusababisha makabiliano na wapinzani wao waliofanya mkutano mkubwa siku ya Jumanne. Katiba ndiyo moja ya sababu kubwa za mfarakano kati ya Mursi na wapinzani wake wasiyoengemea upande wa dini. Baadhi yao wamesusa baraza la kutunga katiba, wakidai kuwa Waislamu wamelaazimisha mtizamo wao kuhusu mustakabali wa Misri mpya.
Lakini muda mfupi baada ya kikao cha mwisho cha baraza la katiba, televisheni ya taifa iliripoti kuwa wajumbe 14 walioondoka kupinga udhibiti wa baraza hilo na wanaharati wa Kiislamu, walirudi kushiriki katika upigaji kura. Moja ya vipengele vitakyopigiwa kura kinazuia maafisa wa ngazi za juu wa chama kilichopigwa marufuku cha rais wa zamani, Hosni Mubarak cha National Democratic Movement, kuwania nafasi yoyote, au kushiriki uchaguzi kwa muda wa miaka kumi.
Mursi kuhodhi madaraka hadi uchaguzi wa bunge
Gazeti la serikali la Al-Ahram limesema kuwa baada ya kuridhia muswada wa katiba hiyo, baraza litauwasilisha kwa rais Mursi, ambaye atapanga tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni mapema wiki ijayo. Baraza hilo limesema mamlaka aliyojipa Mursi yatakabidhiwa kwa bunge baada ya kuridhiwa kwa katiba hiyo.
Laazima kuwepo na katiba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa bunge na hadi hilo lifanyike, rais ataendelea kuhodhi mamlaka ya urais na ya bunge. Uchaguzi wa bunge unaweza kufanyika mapema mwaka ujao.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman