Museveni aongeza siku 21 za kutotoka nje
14 Aprili 2020Raia wa Uganda watasubiri kwa muda wa siku 21 zaidi kuona kama serikali itawaruhusu kurejelea maisha yao ya kawaida. Hii ni kufuatia agizo la rais Yoweri Museveni kuendeleza hatua zilizowekwa wiki mbili zilizopita ikiwemo amri ya kutotoka nje kati ya saa moja jioni hadi kumi na mbili asubuhi.
Leo ndiyo ilikuwa siku ya 14 ya kipindi cha kutotoka nje saa za jioni hadi asubuhi kilichoagizwa na rais Museveni. Waganda wengi walikuwa na matarajio tofauti kuhusu kama amri hiyo ingeondolewa ili waendelee na shughuli zao za kila siku kusaka riziki zao. Lakini rais Museveni ameongezea muda huo akisema bado watachukua tahadhari kuthibitisha hali halisi ya ugonjwa wa COVID-19 nchini Uganda.
Ikilinganishwa na mataifa jirani ya Kenya na Rwanda Uganda ingali ina idadi ya chini ya wagonjwa waliothibitishwa kuungua ugonjwa wa Covid-19. Hadi sasa watu 54 ndiyo wamegunduliwa kuwa na ugonjwa huo tangu mgonjwa wa kwanza alipobainika tarehe 21 mwezi Machi.
Wizara ya afya imeendelea na shughuli za kuwapima watu waliowekwa katika karantini na kutokana na zoezi hilo, watu takribani 40 wamegunduliwa kuwa na virusi hivyo. Ila kuna kundi la karibu watu 18,000 ambao serikali inasema ingali ina wasiwasi nao. Waliingia nchini kati ya tarehe 7 na tarehe 22 mwezi Machi.
Kuna hofu kuwa wanaweza kuwambukiza wengi kwa kuwa hali yao ya afya haijulikani. Mwito umetolewa kwa watu hao kujisalimisha lakini wengi bado hawajajitokeza.
Ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea eneo la Afrika Mashariki, rais Museveni amelegeza kidogo kanuni kwa waendeshaji wa magari ya mizigo kutoka mataifa jirani. Hawatabaki katika karantini ila baada ya kupimwa wataendelea na safari zao huku walichunguzwa na kupata matokeo ya afya yao baadaye.
Hatua hii imeleta nafu kwa waendeshaji walio kwama kwenye mipaka ya Uganda na mataifa jirani. Kwa mfano kule Mpondwe kwenye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, waendeshaji walikuwa wameamua kufanya mgomo kupinga kile walichokitaja kuwa uonevu na kunyanyaswa na maafisa wa uhamiaji.
Hata hivyo waendeshaji wameagizwa kuegesha magari yao maeneo maalum wakiwa safarini bila kutangamana na watu wengine. Hadi waendeshaji 372 waliopimwa kwenye mipaka kuanzia jana Jumatatu. Hawakugunduliwa kuwa na virusi vya Corona.
Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.