1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni kufufua shirika la ndege la Uganda

Mohammed Abdulrahman
7 Juni 2018

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema taifa hilo la Afrika Mashariki litalifufua shirika lake la ndege, ili liweze  kushiriki katika biashara ya usafiri wa anga inayozidi kukua katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/2z5eL
Uganda Präsident Yoweri Museveni
Picha: picture-alliance/dpa/I. Langsdon

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema taifa hilo la Afrika Mashariki litalifufua shirika lake la ndege, ili liweze  kushiriki katika biashara ya usafiri wa anga inayozidi kukua katika eneo hilo, pamoja na kuimarisha sekta yake ya huduma.

Rais Museveni aliyasema hayo katika hotuba yake bungeni jana  lakini hakutaja ndege zitaagizwa kutoka kampuni gani. Waziri wa usafiri na kazi aliwahi kuviambia vyombo vya habari kwamba serikali imeagiza ndege kutoka kampuni ya Canada ya Bombardier.

Museveni amesema kila mwaka Waganda wanatumia dola milioni 430 katika safari za anga, hali inayopaswa kusitishwa.

Uganda inajenga uwanja wa ndege wa pili wa kimataifa na uwanja wake wa kwanza wa kimataifa uliopo mjini Entebbe, kusini mwa mjini mkuu wa Kampala unapanuliwa ili kuweza kupokea abiria wengi zaidi pamoja na usafirishaji wa mizigo. Mradi huo wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Entebbe unatumia fedha za mkopo kutoka China.