Musharraf aikimbia Mahakama
18 Aprili 2013Kukimbia kwa Pervez Musharaf katika mahakama moja mjini Islamabad imeonesha wazi kupungua kwa umaarufu wa mkuu huyo wa zamani wa jeshi la pakistan ambaye aliwahi kuvuma sana katika ulingo wa kisiasa, sasa azma yake ya kutaka kurudi tena katika siasa za nchi hiyo zimedidimizwa kutokana na kibali cha kukamatwa kwake.
Mahakama iliamuru kukamatwa kwa Musharraf kutokana na makosa aliyoyafanya mwaka wa 2007 alipokuwa madarakani ya kuwafuta kazi majaji watatu na kutaka kuwaweka katika kifungo cha nyumbani. Hatua ambayo inasemekana kuwa kinyume cha katiba ya Pakistan.
Kiongozi huyo wa zamani alikuepo mahakamani wakati uamuzi wa kukamatwa kwake ulipotolewa. Musharaf aliondoka mahakamani mara moja akisindikizwa na walinzi wake hadi katika gari lake na kuondoka. Licha ya kibali hicho kutolewa hakuna polisi hata mmoja aliyojaribu kumzuia kuondoka katika mahakama hiyo.
Haijawa wazi Musharraf atakamatwa lini
Mamia ya wafuasi wake waliokuepo nje ya mahakama hiyo walisema kwa sauti "hii sio haki, Maisha marefu kwako Musharaf ". Wafuasi hao bila shaka walikuwa wanapinga hatua ya mahakama ya kuamuru kukamatwa kwa kiongozi wao.
Kwa sasa haijawa wazi ni lini jenerali huyo mstaafu atakapokamatwa. Kulingana na msemaji wa chama chake Mohammad Amjad, kiongozi huyo atawasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kupinga amri ya kukamatwa kwa Pervez Musharraf.
Musharraf pia anakabiliwa na mashitaka ya kupanga njama ya mauwaji ya kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto mwaka wa 2007, na kuhusiana na kifo cha kiongozi wa waasi kabila la Baluch wakati wa operesheni ya kijeshi mwaka wa 2006.
Nawaz Sharif aonekana kuchukua uongozi
Rais huyo wa zamani alirudi nyumbani tarehe 24 mwezi uliopita,baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka minne nchini Dubai na Uingereza, na kuahidi kugombea katika uchaguzi mkuu unaoratajiwa kufanyika Mai 11 mwaka huu.
Hata hivyo matarajio yake ya kusimama tena katika uchaguzi mkuu ujao yalizimwa baadaye wiki hii baada ya maafisa wa uchaguzi kumuondoa katika nafasi hiyo wakisema Musharraf anakabiliwa na changamoto kubwa katika kesi zinazomkabili.
Pervez Musharaf alichukua madaraka kutokana na mapinduzi ya serikali ya Pakistan mwaka wa 1999 na kuachia ngazi mwaka wa 2008. sasa waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif ambaye aliondolewa madarakani kutokana na mapinduzi yaliofanyika anaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman