1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf akabili changamoto Pakistan

10 Mei 2007

Jamadari Musharraf wa Pakistan akabili changamoto kali kutoka wapinzani wake nchini na mahkamani kwa kumsimamisha kazi hakimu Chaudhry.

https://p.dw.com/p/CHEV

Licha ya hasira za watu,kukosolewa na vyombo vya habari na upinzani takriban kutoka mahkama nzima-mambo yaliopunguza umaarufu na nguvu zake ,rais Parvez Musharraf wa Pakistan, anan’gan’gania kumtimua hakimu mkuu.

Miezi kadhaa kabla uchaguzi kufanyika nchini Pakistan,rais Musharraf amejiharibia jina kwa kumsimamisha kazi hakimu mkuu Ifikhar Chaudhry hapo machi 9 kutokana na mashtaka yasiotajwa hadharani ya ukosefu wa nidhamu.Hayo ni mashtaka ambayo watu wengi nchini Pakistan, wanatuhumu ni njama tu za kisiasa.

Mhariri wa gazeti la TIMES la Pakistan Najam Sethi amesema na ninamnukulu, “Amepoteza mamlaka yake mengi.Atapaswa kuamua sasa vipi atamudu kun’gania madaraka aliosalia nayo.”

Sethi anaamini janerali musharraf anavutwa na wimbi la ama kuchagua kugawana madaraka na mpinzani wa kiraia mfano wa waziri mkuu wa zamani aishie uhamishoni Benazir Bhutto au kutawala binafsi kimabavu.

Shida iliopo ni kuwa Bhutto, hangeonesha kuridhia mpango kama huo na angedai bei kubwa zaidi kuliko kabla Musharraf hajajitosa katika balaa hili la kumtimua hakimu mkuu.

Mwishowe, Musharraf atabidi kuacha wadhifa wa mkuu wa majeshi.

Wachambuzi wa kisiasa hawako pekee yao katika kutia shaka iwapo Musharraf sahibu wa Marekani ataweza tena kujipatia umaarufu aliokuwanao katika dola hili linaloyumbayumba lka kiislamu kabla hakumtimua hakimu huyo.

Mama mmoja mzee huko Islambad alinun’gunika hivi:

“Amezicheza karata zake vibaya sana .Angeliweza kuikoa nchi.”

Siku hizi Bibi Parveen anahisi tofauti kabisa juu ya jamadari huyu ambae alimuwekea matarajio makubwa aliponyakua madaraka 1999 na kukomesha mwongo wa utawala wa kiraia uliokatisha watu tamaa.

Hakimu Chaudhry asieelemea upande wowote ameshapata imani ya umma wa watu kwa msimamo wake mkamavu isipokuwa serikali na vyombo vyake vya dola.

Ni hakimu aliethubutu kushughulikia kesi za wafungwa waliotoweka bila kujulikana hatima zao na aliepinga kuuzwa kwa kiwanda cha chuma mali ya serikali.

Chaudhry mwenye umri wa miaka 58,amekuwa akijizuwia sasa kutoa matamshi ya kisiasa huku akiitaka jamii ya wanasheria kutetea uhuru wa mahkama na wa katiba.

Shirika la mawakili nchini Pakistan linalompigania hakimu Chaudhry, limepania nalo kupepea bendera na kuendeleza shinikizo.

Wachambuzi wanahisi kwamba jamadari Musharraf angependelea hakimu mkuu mwengine anaeweza kumyumbisha ashughulikie mageuzi ya katiba ambayo yaweza kupendekezwa na wapinzani.

Sasa chochote kile ambacho jamadari musharraf atachotenda ,hatua yake itakayokuja katika mvutano huu ,kitakumbana na hatari.

Ikiwa hatafaulu kufikia muafaka na waziri-mkuu wa zamani Benazir Bhutto na akachukua hatua ya kimabavu badala yake, Musharraf ataudhi umma wa wapakistan.

Atawafanya washirika wake wa Marekani kufikiri mara mbili iwapo ni kiongozi mwenye uwezo kweli wa kuiongoza Pakistan, kufuata mkondo wa siasa wastani na demokrasia.