1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakabali wa mazungumzo ya Brexit kujulikana Jumapili

10 Desemba 2020

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson pamoja na rais wa kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen wamekubaliana siku ya Jumapili kuwa ndio mwisho wa majadiliano ya mustakabali wa makubaliano ya baada ya Brexit.

https://p.dw.com/p/3mVYA
EU Brexit-Verhandlungen in Brüssel
Picha: Olivier Hoslet/AFP

Ni makubaliano yanayofuatia mazungumzo yao ya masaa matatu sambamba na chakula cha jioni kutozaa matunda. 

Johnson alikwenda Brussels jana Jumatano, katika juhudi za mwisho mwisho za kunusuru mazungumzo hayo ya kibiashara ambayo yanaelekea kushindwa na hatimaye viongozi hao wawili kukubaliana kwamba wawakilishi wao kwenye mazungumzo hayo watatakiwa kujaribu kwa mara nyingine kuondoa mkwamo uliopo.

Von der Leyen amesema kwenye taarifa yake baada ya mazungumzo hayo makao makuu ya umoja huo mjini Brussels kwamba walikuwa na mazungumzo yenye tija kuhusiana na masuala tata yaliyosalia na kuongeza kuwa walielewana kuhusu msimamo wa kila mmoja kwenye masuala hayo, na kukiri bado kuna tofauti kubwa.

Chanzo kimoja cha ngazi za juu cha Uingereza pia kimesema kwamba tofauti bado ni kubwa na haijulikani iwapo kuna uwezekano wa pande hizo mbili kufikia muafaka.

Vingozi hao wamekubaliana kujadiliana zaidi kupitia timu zinazoshiriki mazungumzo hayo katika siku chache zijazo na kwamba maamuzi magumu yatatakiwa kuchukuliwa siku ya Jumapili, kimeongeza chanzo hicho.

Belgien Michel Barnier und David Frost
Wakuu wa wajumbe wa mazungumzo ya Brexit, Michel Barnier wa umoja wa Ulaya na David Frost wa uingerezaPicha: Oliver Hoslet/REUTERS

Je wawakilishi watafanikisha kupatikana suluhu?

Kiongozi wa mazungumzo hayo kutoka upande wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier pamoja na mwenzake wa Uingereza David Frost walijaribu kuzipunguza tofauti kati ya pande hizo katika kipindi cha miezi minane lakini London inasisitiza kwamba taifa hilo litataka uhuru wake kamili ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Vyanzo kutoka Ulaya vimesema watu wawili hao na timu zao wamerejea kwenye majadiliano asubuhi ya leo, kabla tu ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa wakuu wa mataifa wanachama wa umoja huo, ambao kwa mara nyingine utagubikwa na kiwingu cha wasiwasi kuelekea ushirikiano baina yao.

Vizingiti vinavyosalia kwenye mazungumzo hayo ni masuala kuhusiana na uwanja sawa wa kibiashara na suala la uvuvi kwenye eneo la maji la Uingereza. Johnson aliwaambia wabunge wa Uingereza kabla ya kuondoka kwamba bado kuna masuala muhimu yanayotakiwa kushughulikiwa, lakini akiwahakikishia wabunge hao kwamba Uingereza itaendelea kung'ara kwa makubaliano ama bila ya makubaliano.

Mjini Berlin, kansela wa Ujerumani alisema jana kwamba bado kuna fursa ya kukubaliana lakini akionya hawatatakiwa kuhatarisha uadilifu uliojengeka wa soko la pamoja. Merkel pamoja na viongozi wengine wa Ulaya ambao ni pamoja na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, watakuwa miongoni mwa wakuu wa Ulaya wanaokutana leo mjini Brussels kwenye mkutano wa kilele, lakini Johnson hakualikwa.

Soma Zaidi: Umoja wa Ulaya, Uingereza zarejea kwenye meza ya mazungumzo

Von der Leyen atawaarifu wanachama hao kuhusu mazungumzo yake na Johnson na kuwaeleza ishara anazoziona kuhusina na mazungumzo hayo na kule yanapoelekea, wanadiplomasia wamesema.

APE/AFPE