1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mustakabali wa Nagorno Karabakh wajadiliwa

21 Septemba 2023

Wajumbe wa jamii ya Warmenia kutoka Nagorno Karabakh na serikali ya Azerbaijan wajadili kuhusu hatma ya jimbo hilo baada ya vita kuzuka upya

https://p.dw.com/p/4WdTT
Maandamano ya Warmenia katika mji mkuu Yerevan
Waarmenia wakipinga operesheni ya kijeshi ya Arzerbaijan dhidi ya Nagorno KarabakhPicha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Wajumbe kutoka jimbo la Nagorno-Karabakh na serikali ya Azerbaijan  wanakutana kwa mazungumzo kujadili mustakabali wa jimbo hilo lililojitenga na ambalo Azerbaijan inadai inalidhibiti kikamilifu hivi sasa baada ya kuendesha operesheni kubwa ya kijeshi wiki hii kwenye eneo hilo. Jamii ya Warmenia katika jimbo hilo inalalamika kwamba wanajeshi  hao wa Azerbaijan wamekiuka makubaliano ya kusitisha vita.

Mazungumzo hayo  yaliitishwa baada ya wanajeshi wa Armenia katika jimbo la Nagorno Karabakh kukubali kuweka chini silaha kufuatia kuzuka upya kwa mapigano hivi karibuni katika mvutano wa miongo kadhaa wa kuwania udhibiti wa jimbo hilo.

Maafisa wa Nagorno Karabakh na shirika la habari la serikali la Azerbaijan wote wameripoti kwamba mazungumzo ya leo katika mji wa Azerbaijan wa Yevlakh, baina ya viongozi wa jimbo hilo  na serikali ya mjini Baku, yatajikita katika kuangalia namna ya kulijumuisha tena jimbo hilo lililojitenga katika nchi ya Arzerbaijan.

Ingawa wakati ikielezwa mazungumzo hayo yameanza, ripoti nyingine zinasema kwamba maafisa wa Armenia wameripoti juu ya kusikika kwa milio ya risasi katikati ya mji mkuu wa jimbo hilo, Stepanakert. Vyanzo viwili vililiambia shirika la habari la Reuters asubuhi kwamba milio ya risasi imesikika.

Mgogoro wasababisha uharibifu Nagorno Karabakh
Magari yaliyoharibiwa katika mji mkuu wa Nagorno-Karabakh Stepanakert Picha: Siranush Sargsyan/PAN Photo via REUTERS

Kadhalika jamii ya Warmenia katika jimbo hilo linalozozaniwa imesema wanajeshi wa Azerbaijan walioko katika eneo hilo wamekiuka makubaliano ya kusitisha vita ingawa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imekanusha madai yaliyotolewa.

Mamlaka ya jimbo hilo linalokaliwa na jamii kubwa ya Warmenia inayoendesha shughuli zake bila ya kutambuliwa kimataifa tangu vilipozuka vita mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1990, jana Jumatano mchana  ilitangaza  kwamba vikosi vyake vya ulinzi vitaweka chini silaha na kuvunjwa chini ya makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Urusi.

Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev alisifu ushindi wa wanajeshi wake kupitia hotuba yake kwa taifa akisema jeshi la nchi yake limeyarejesha mamlaka ya jimbo la Nagorno Karabakh.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano wa dharura kufanyika leo alhamisi kufuatia ombi la Ufaransa, kuhusiana na operesheni hiyo ya Azerbaijan. Armenia imeuonya Umoja wa Mataifa kwamba Azerbaijan inaendesha harakati za takasatakasa ya kikabila  katika jimbo hilo la Nagorno Karabakh.

Rais  Ilham Alijev akitowa hotuba kwa taifa
Rais wa Arzerbaijan Ilham AlijevPicha: Press Service of the President of Azerbaijan Ilham Alijew/REUTERS

Mjumbe wa haki za binaadamu katika jimbo la Nagorno Karabakh Ombudsman Geghan Stepanyan amesema  kiasi watu 200 wakiwemo raia 10 waliuwawa na zaidi ya wengine 400 walijeruhiwa kwenye mapigano na watoto wametajwa kuwa miongoni mwa waliouwawa na waliojeruhiwa.Ingawa idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa na vyombo huru.

Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan nae kwenye hotuba yake amesema Wanajeshi wa kulinda amani wa Urusi ndio wenye kuwajibika kikamilifu na usalama wa watu wa Nagorno Karabakh. Jana Waarmenia walimiminika kwenye mji mkuu wa nchi yao wa Yerevan kwa siku ya pili mfululilizo wakidai maamlaka ziwatetee Waarmenia wa Nagorno Karabakh.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW