1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muturi: Mwanangu ni muhanga wa utekaji Kenya

Sylvia Mwehozi
13 Januari 2025

Mwanasheria Mkuu wa zamani katika serikali ya Rais William Ruto wa Kenya, Justin Muturi amekuwa wa kwanza kuzungumzia wimbi la utekaji nyara vijana wanaoikosoa serikali, akisema mwanae wa kiume ni muathirika wa utekaji.

https://p.dw.com/p/4p6Nl
Nairobi Kenya | Waandamanaji
Waandamanaji wanaopinga matukio ya utekaji KenyaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Justin Muturi, ambaye alihudumu kama mwanasheria mkuu katika serikali ya Ruto tangu mwezi Oktoba mwaka 2022 hadi Julai 2024, siku ya Jumapili alizungumzia suala la utekaji ambalo limewaandama Wakenya kwa miezi kadhaa.

Kulingana na Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Kenya, watu wasiopungua 82 wametekwa na vikosi vya usalama tangu kufanyika maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana mwezi Juni, huku kadhaa wakiwa bado hawajalikani walipo.

Muturi, alisema katika taarifa yake kwamba "kumekuwa na visa vya utekaji nyara na baadhi ya vifo ambavyo havijatolewa maelezo tangu kuzuka kwa maandamano ya GenZ mwaka jana".

Soma pia:Hatimaye Ruto aahidi kukomesha utekaji raia

Ameendelea kueleza kwamba yeye pia ni mwathirika wa kadhia hiyo baada ya mwanae wa kiume kutekwa na kutoweka na hakuwa na uhakika kama alikuwa amekufa au yu hai.

Licha ya kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Kitaifa wakati ambao mwanae alitekwa nyara, Muturi alisema hakuweza kupata taarifa zozote kuhusu aliko mwanawe.

Baadae aliachiliwa na "maafisa wasiojulikana" na hakushitakiwa. Vijana wengine watano waliachiliwa wiki iliyopita bila maelezo yoyote kutoka kwa mamlaka.

Kutekwa kwa mwanaharakati wa Tanzania nchini Kenya

Wakati afisa huyo mwandamizi akitoa maoni yake, siku ya jumapili Kenya iliandamwa tena na wimbi la utekaji, baada ya mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini Tanzania Maria Sarungi Tsahai, kuripotiwa kutekwa mchana wa Jumapili, katika mitaa ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kabla ya kujitokeza na kusema kwamba yuko salama.

Waandamanaji kadhaa watiwa mbaroni Kenya

Shirika la Kimataifa la Amnesty International tawi la Kenya lilisema kuwa Tsehai "alitekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha na kupakiwa kwenye gari nyeusi aina ya Toyota Noah" majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Kilimani katikati mwa Nairobi.

Soma pia:Hasira zaongezeka Kenya kuhusiana na utekaji wa wakosoaji

Mtafiti wa Amnesty International Roland Ebole alisema kutekwa nyara kwa Sarungi Tsehai ni mfano mwingine wa "ukandamizaji wa kimataifa unaofanyika katika ardhi ya Kenya," shutuma ambazo mamlaka za Kenya zinakanusha. Kenya imekuwa na historia ya kuruhusu serikali za kigeni kuwateka nyara raia wao na kuwarudisha kwa lazima kinyume na sheria za kimataifa.

Mnamo mwezi Oktoba, Umoja wa Mataifa ulielezea "wasiwasi mkubwa" juu ya ripoti kwamba wakimbizi wanne wa Kituruki walitekwa nyara jijini Nairobi na kurudishwa Uturuki kwa lazima.

Mwezi Novemba, kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alitekwa nyara jijini Nairobi na kurejeshwa kwa lazima kampala anakokabiliwa na mashitaka katika mahakama ya kijeshi.