Hatua hii inapisha shughuli ya kuunda kamati ya operesheni za bunge iliyo na wajibu wa kuchagua kamati ya uteuzi itayoanzisha mchakato wa kuwapiga msasa mawaziri wapya. Hili linafanyika ikiwa imepita wiki moja tangu bunge la taifa kufunguliwa rasmi.
Vurugu zilizuka bungeni pindi baada ya tangazo la viongozi wapya kutangazwa. Kwenye kikao cha alasiri, spika Moses Wetangula aliweka bayana majina ya viongozi wapya wa bunge.
Kimani Ichungwa ambaye ni mbunge wa Kikuyu ndiye mwakilishi wa chama tawala bungeni na naibu wake ni mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya.
Kiongozi wa upinzani bungeni ni Opiyo Wandayi ambaye ni mbunge wa Ugunja kutoka muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na naibu wake ni mbunge wa Kathiani Robert Mbui.
Kiranja wa bunge ni mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro na naibu wake ni mbunge wa viti maalum Naomi Waqo. Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula amesisitiza kuwa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya hauna mbunge yeyote aliyechaguliwa kupitia chama hicho.
Wetangula alitilia mkazo kuwa wawakilishi wa walio wengi sharti awe kiongozi wa chama au muungano wa vyama vilivyoko bungeni.
Viongozi wa Seneti walikwishatangazwa
Wakati huo huo, Spika wa Senati Amason Kingi alitangaza rasmi mwanzoni mwa wiki majina ya viongozi wa baraza hilo kwenye kikao cha kwanza tangu kufunguliwa rasmi.
Kwa upande mwengine, Rais William Ruto amewasilisha rasmi orodha ya majina ya mawaziri wapya watakaokaguliwa na bunge la taifa.
Kwenye kikao cha alasiri, Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula aliwasilisha ujumbe huo ulioweka bayana majina 22 ya baraza jipya la mawaziri na mwanasheria mkuu Justin Muturi.
Mchakato wa kuwapiga msasa na kutoa ridhaa mawaziri watarajiwa sharti ukamilike katika kipindi cha siku 28 kutokea siku ya kuarifiwa.
Hilo litaipisha shughuli ya kuunda kamati ya bunge ya operesheni itakayopendekeza majina ya wanachama wa kamati ya uteuzi.
Yote hayo yakiendelea, tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC, imetangaza kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa uchaguzi mdogo wa wabunge kwenye wadi 5 utafanyika tarehe 8 mwezi wa Disemba.